Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (wa kwanza kutoka kulia) akikagua moja ya transfoma itakayofungwa katika kituo kipya cha kupoza umeme cha Mtera wakati wa ziara ya kukagua Miundombinu ya Bwawa la Mtera,Mitambo ya Kuzalisha pamoja na Kituo cha Kupoozea Umeme ”Substation”.
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (wa kwanza kutoka kulia) akikagua moja ya transfoma itakayofungwa katika kituo kipya cha kupoza umeme cha Mtera wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua Miundombinu ya Bwawa la Mtera,Mitambo ya Kuzalisha pamoja na Kituo cha Kupoozea Umeme ”Substation”.
Kaimu Mhandisi Mkuu katika Kituo cha kufua umeme cha Mtera, Phesto Chikongoye (kushoto) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato kuhusu uendeshaji wa mitambo mbalimbali ya umeme katika kituo hicho wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua Miundombinu ya Bwawa la Mtera,Mitambo ya Kuzalisha pamoja na Kituo cha Kupoozea Umeme ”Substation”.
Baadhi ya mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo katika kituo cha kufua umeme cha Mtera .
Baadhi ya mitambo ya umeme katika kituo cha kupoza umeme cha Mtera
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (aliyenyoosha mkono) akitazama moja ya mashine za kuzalisha umeme katika Kituo cha kufua umeme cha Mtera ambayo imewekwa kama spea katika kituo hicho wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua Miundombinu ya Bwawa la Mtera,Mitambo ya Kuzalisha pamoja na Kituo cha Kupoozea Umeme ”Substation”.
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Nhinhi wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma wakati alipofika kijijini hapo kukagua kazi ya usambazaji umeme.
…………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Mtera
Serikali imeagiza ujenzi wa upanuzi wa kituo cha kupozea umeme cha kV 220/33 kwenye kituo cha kufua umeme Mtera kukamilika kabla ya mwezi Octoba mwaka huu.
Maagizo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Wakili Stephen Byabato wakati alipofanya ziara ya kukagua uzalishaji wa kituo cha kufua cha umeme kwa maji Mtera amesema lazima kikamilike kwa wakati ili kuongeza umeme hasa vijiji jirani kwa Mikoa ya Iringa na Dodoma
“Tunapanua kituo cha kupoza umeme kilichopo hapa ili kukiongezea nguvu na hivyo kuweza kusambaza umeme katika Mkoa wa Iringa na Dodoma, kazi ilichelewa kidogo kutokana na masuala mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa vifaa vya umeme kutoka nje ya nchi, hivyo nimetoa maelekezo kuwa Mkandarasi anatakiwa kufanya kazi usiku na mchana,” amesema Wakili Byabato.
Upanuzi wa kituo hicho unafanywa chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambao umelenga kuzalisha megawati 20 zitakazoelekezwa katika vijiji vya mikoa ya Iringa na Dodoma.
Naibu Waziri Byabato amesema tayari baadhi ya kazi zimeshafanyika katika kituo hicho kipya cha kupoza umeme ikiwemo ujenzi wa miundombinu na ufikishaji wa transfoma na vifaa vingine vya umeme vinavyohitajika katika kazi hiyo yote ni kuhakikisha kinakamilika kwa wakati.
Kuhusu hali ya uzalishaji umeme katika Kituo cha Mtera, Wakili Byabato amesema kuwa, kituo hicho kinazalisha megawati zote 80 kutoka katika mitambo miwili iliyopo kituoni hapo ambapo kila mtambo unazalisha megawati 40, hivyo aliwapongeza watalaam wa TANESCO kwenye kituo hicho kwa kufanya kazi kwa weledi, kujituma na ubunifu.
Amebainisha kuwa, kuna maji ya kutosha kuzalisha umeme katika bwawa la Mtera, yenye kina cha mita 698.50 na kwamba maji yaliyopo yana uwezo wa kuzalisha umeme katika kipindi cha mwaka mzima hata kama mvua hazitanyesha.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Jones Olotu, amesema kuwa, watamsimamia mkandarasi aliyepewa kazi ya upanuzi wa kituo kupoza umeme cha Mtera ili kuhakikisha kuwa kazi husika inakamilika mapema kama ilivyoagizwa na Naibu Waziri.
Nae Meneja wa Kituo cha Kufua Umeme kwa maji Mtera, Elias Mwalupilo amesema hali ya mtiririko wa maji kwenye bwawa hilo kwa miaka miwili umekuwa ni mzuri.
“ Kwa kiwango cha maji kilichopo, hata kama mvua hazitanyesha yanaweza kuzalisha umeme bila shida kwa mwaka mzima mvua za masika na vuli zimemalizika ila maji haya yanaweza tufikisha mpaka masika ya mwakani.” amesema.
Amebainisha kuwa wanatarajia kufanya ukarabati mkubwa wa mitambo ya Kituo Cha Mtera Septemba na Oktoba mwaka huu, ukarabati ambao utahusisha kuzima mtambo mmoja.
“ Tutafanya kwa awamu na tutazima mtambo, lakini tumejiandaa kwa ukarabati huu ambao hautaathiri upatikanaji wa umeme.” amesema.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Nishati, alikagua kazi ya ujenzi wa miundombinu ya umeme katika kijiji cha NhiNhi kilichopo wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma na kumuagiza mkandarasi, kampuni ya A to Z, kupeleka umeme kwenye kijiji hicho kabla ya tarehe 30 Juni mwaka huu, na umeme huo ufike kwenye Taasisi zote za umma ikiwemo Shule na Kituo cha Afya.