…………………………………………………………………….
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile amefuturisha wananchi wa eneo la Kibaigwa wilayani Kongwa Dodoma katika msikiti wa Kibaigwa ambapo amewaomba kutumia Mwezi huu kuliombea Taifa na serikali yake.
” Niwashukuru kwa kukubali kupokea Sadaka yangu ya Iftari, niwaombe katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu tuzielekeze pia funga zetu katika kuiombea Nchi yetu na Rais wetu Mama Samia ambaye ameonesha kuanza utendaji wake kwa kasi na unaoridhisha akisisitiza umoja na mshikamano kwetu sisi sote kama Taifa.
Ninafahamu mnataka kuanza ujenzi wa jengo kubwa la Msikiti hapa Kibaigwa, niko tayari kushirikiana nanyi katika kufanikisha ujenzi wa nyumba hii ya Mwenyezi Mungu, tutaanza pamoja na Inshallah naamini tutafanikisha,” Amesema Mbunge Ditopile.
Kwa upande wake Imamu wa Msikiti huo, Sheikh Salum Salum amemshukuru Mbunge Ditopile kwa sadaka hiyo ya Futari huku akimhakikishia wao kama viongozi wa Dini wataendelea na wajibu wao wa kuiombea serikali, Rais Mama Samia, wabunge pamoja na kuhubiri amani na mshikamano kama ambavyo Rais Samia amekua akisisitiza.
” Tunakushukuru kwa kutuandalia Iftari kwenye Mwezi huu Mtukufu, hakika kama alivyosema Mtume Muhammad yeyote ambaye atawashibisha watu katika mfungo wa Ramadhan basi hakika amesamehewa madhambi yake yote, kama viongozi wa Dini tutaendelea kuwaombea viongozi wetu na Mungu awaongoze,” Imamu wa Msikiti wa Kibaigwa, Shehe Salum Salum.