Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Lughano J.M. Kusiluka, akizindua kongamano la “Career Fair” lililofanyika Chuo Kikuu Mzumbe na kushirikisha wanafunzi na Chuo hicho na Chuo cha Kilimo Sokoine.
Baadhi ya wanafunzi wakisikiliza kwa makini mada zilizokuwa zikifundishwa wakati wa Kongamano la “Career Fair” Mzumbe.
Mgeni rasmi Prof. Prof. Lughano J.M. Kusiluka, akitembelea sehemu ya maonesho ya huduma mbalimbali zinazonunuliwa kwa huduma ya mtandao kupitia Benki ya NMB wakati wa Kongamano la “Career Fair”
Baadhi ya washiriki wa Kongamano la “Career Fair” wakiwa kwenye picha ya pamoja na mgeni rasmi na viongozi wa Benki ya NMB
*********************************
Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini wametakiwa kuwa wabunifu na wadadisi ili kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na wadau mbalimbali wa Sekta ya Elimu, kwa lengo la kuwawezesha kuendana na mabadiliko ya Mapinduzi ya Nne ya Viwanda duniani“ 4th Industrial Revolution”.
Ushauri huo umetolewa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Lughano J.M. Kusiluka, kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe na Sokoine wakati akifungua Kongamano la Career Fair 2021, lililodhaminiwa na Benki ya NMB kwa ushirikiano na Shirika la AIESEC Tanzania.
Prof. Kusiluka amesema kongamano la “Career Fair” kwa mwaka 2021 limekuja wakati muafaka, kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana, hususani suala la ukosefu wa ajira pindi wanapohitimu masomo yao.
Amesema “Kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani na ukosefu wa ajira kwa vijana ni changamoto kubwa ambayo imeendelea kutuumiza vichwa katika kupambanua nini hatma ya wahitimu wetu, na kwamba hatuna budi kubadilisha mfumo wa ufundishaji ili uendane na mahitaji halisi ya soko, ya kuzalisha wataalamu wabobevu na wabunifu, ambao wataweza kujiajiri wenyewe mara wanapohitimu, badala ya kusubiri kuajiriwa”. alisisitiza
Ameipongeza Benki ya NMB na Shirika la AIESEC, kwa uwekezaji mkubwa walioufanya kwa vijana kupitia programu ya “Career Fair” ambayo imelenga kumjenga na kumkomboa kijana kifikra. Ameahidi Chuo Kikuu Mzumbe kuendelea kubuni mikusanyiko ya aina hiyo yenye kulenga kuwajengea uwezo vijana na fursa zilizopo; pamoja na kuendeleza mpango wake wa kuimarisha kituo cha kuatamia bunifu za wanafunzi chini ya Skuli ya Biashara, kwa lengo la kuwaanda vijana kujiajiri.
Akizungumza wakati wa Kongamano hilo, Mkuu wa Kanda ya Mashariki NMB, Ndugu. Dismas Prosper, amesema Benki ya NMB imedhamini Kongamano hilo ili kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana, kuibua vipaji na kufungua fursa za mafunzo ya kazi kupitia programu yake ya ” Career development” ambayo inatoa fursa kwa vijana waliohitimu vizuri mafunzo yao kupata uzoefu wa kazi na hata kuajiriwa katika benki hiyo kulingana na fursa zilizopo.
Amesema hadi sasa chini ya mpango huo Benki ya NMB imewawezesha zaidi ya vijana 50 kujengewa uwezo, kupata ujuzi na kujifunza kazi kwa vitendo, huku baadhi yao wakiwa wameajiriwa na Benki hiyo kwa nafasi mbalimbali.
“ Programu hii tutaiendeleza kwa vyuo vikuu vyote nchini kwa lengo la kuibua vipaji na ubunifu ili tutimize azma yetu ya kuendelea kuwa Benki Bora ya vijana” alisisitiza.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la AIESEC Tawi la Tanzania, Bw. Michael Chacha, amesema Shirika lake litaendelea kuwajengea uwezo vijana wahitimu wa Elimu ya Juu ili kusaidia kupunguza changamoto za ajira pamoja na kuendelea kutoa mafunzo ya namna mbalimbali kwa vijana kupia washirika wake wa ndani na nje, ili kuandaa viongozi wenye uwezo kusaidia maendeleo ya Taifa.
Kongamano la “ Career Fair” limefanyika Chuo Kikuu Mzumbe -Morogoro, na kuwashirikisha vijana zaidi 1000, ambao walipata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali kuhusu ujasiriamali, uongozi, biashara ajira, ubunifu na Teknolojia. Mafunzo hayo yalitolewa na wataalamu mbalimbali wakiwemo wa Benki ya NMB na AIESEC Tanzania.