Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga akizungumza wakati alipofungua Kongamano la kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wanafunzi wenye Ulemavu na Maendeleo lililokuwa na kauli mbiu isemayo “Ulemavu si Kukosa Uwezo” kwenye Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Mei 8, 2021 Jijini Dodoma.
Sehemu ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (hayupo pichani) wakati wa Kongamano la kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wanafunzi wenye Ulemavu na Maendeleo lililofanyika katika chuo Kikuu cha Dodoma.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya Mhe. Fatuma Taufiq akielezea masuala mbalimbali kuhusu Ugonjwa wa Ukimwi wakati wa kongamano hilo. Kushoto ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Nderiananga.
Kiongozi wa Wanafunzi wenye Ulemavu Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Bw. Kelvin Mkude akisoma risala wakati wa kongamano hilo lililowakutanisha kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wanafunzi wenye Ulemavu na Maendeleo lililokuwa na kauli mbiu isemayo “Ulemavu si Kukosa Uwezo” kwenye Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Mei 8, 2021 Jijini Dodoma
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Nderiananga akigawa Vifaa Visaidizi kwa Wanafunzi wenye Ulemavu waliopo kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma mara baada ya kufungua Kongamano hilo.
PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
**********************
Na: Mwandishi Wetu – Dodoma
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga ameitaka jamii kuwapatia watu wenye ulemavu nafasi ya kuonyesha uwezo walionao katika kuleta maendeleo kwenye maeneo yanayowazunguka.
Ameeleza hayo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wanafunzi wenye Ulemavu na Maendeleo lililokuwa na kauli mbiu isemayo “Ulemavu si Kukosa Uwezo.”
Alieleza kuwa Sera ya Taifa ya maendeleo na huduma kwa watu wenye ulemavu yam waka 2004, Sheria ya Watu wenye ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 na Mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu 2006 imeeleza suala la ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika shughuli mbalimbali ikiwemo elimu, siasa, shughuli za uzalishaji mali, michezo pamoja na utamaduni.
“Watu wenye Ulemavu wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi kwa weledi na kwa ufanisi pamoja na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo endapo watapewa fursa na kushirikishwa kikamilifu, hivyo ni juku letu sote kuendelea kuelimisha jamii kuondokana na fikra potofu juu ya Watu wenye Ulemavu” alisema Naibu Waziri Ummy
Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuyapa kipaumbele masuala ya watu wenye ulemavu katika nyanja mbalimbali na kwa kutambua uwezo mkubwa wa utendaji kazi waliokuwa nao wenye ulemavu.
“Kwa kutambua uwezo mkubwa waliokuwa nao watu wenye ulemavu Mheshimiwa Rais amefanya teuzi mbalimbali za uongozi kwa watu wenye ulemavu na hivyo ushirikishwaji pamoja na ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo imekuwa ikiimarika siku hadi siku,” alieleza
Alifafanua kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu shughuli za Watu wenye Ulemavu nchini kwa kuzingatia Sera, Sheria, Miongozo na Mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020 – 2025, Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Taifa ya Mwaka 2030 na Mpango wa Tatu wa Taifa wa Miaka Mitano 2021 – 2026.
Pia, alieleza kuhusu utoaji wa mafunzo ya stadi za kazi na huduma za marekebisho kwa watu wenye ulemavu katika vyuo mbalimbali vinavyosimamiwa na Ofisi hiyo ikiwemo Chuo cha Yombo – Dar es Salaam, Sabasaba – Singida, Masiwani – Tanga, Luanzari – Tabora, Mirongo – Mwanza na Mtapika – Masasi pamoja na kuwashirikisha kikamilifu watu wenye ulemavu kwenye Programu ya Taifa ya Ukuzaji Ujuzi.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ummy alielezea juhudi za serikali katika kuboresha miundombinu na kujenga mazingira mazuri na fikivu ya kuwawezesha watu wenye ulemavu wanapata mahitaji yao kulingana na hali zao.
Sambamba na hayo aliupongeza uongozi wa chuo cha Dodoma (UDOM) kwa kuunda kitengo maalum kinachoshughulikia masuala ya Wanafunzi wenye Ulemavu pamoja na kuyapa kipaumbele mahitaji yao muhimu ya kielimu ikiwemo vifaa saidizi.
“Napenda kupongeza Uongozi wa Chuo cha UDOM kwa kutambua mchango wa wenzetu wenye ulemavu katika kupata haki saw ana fursa zinazostahili kama wengine,”
Aidha, aliwasihi vijana wenye ulemavu waliopo chuoni hapo kutambua kuwa wanamchango mkubwa wa kuchangia katika jamii na taifa kwa ujumla, hivyo wasichukulie kuwa na ulemavu siyo kutokuweza.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mhe. Fatuma Taufiq ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya aliwaasa wanafunzi hao kuchukua taadhari dhidi ya Ukimwi na Madawa ya kulevya ili waweze kutimiza malengo yao.
“Takwimu zinaonyesha vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 wapo kwenye mazingira hatari ya kupata maambuki mapya ya Ukimwi, hivyo ni vyema mkachukua taadhari ili mjikinge dhidi ya janga hilo,” alieleza Taufiq
Akizungumza kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Julius Nyahongo alieleza kuwa Chuo hiko kimekuwa kikizingatia suala la ujumuishwaji wa Watu wenye Ulemavu ambapo jumla ya wanafunzi 76 wapo chuoni hapo wakiendelea na masomo katika fani mbalimbali.
Naye, Mkurugenzi wa Elimu Maalum kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Stadi Dkt. Magreth Mtonya alisema kuwa Serikali imeendelea kuweka kipaumbele cha upatikanaji wa vifaa visaidizi kwa watu wenye ulemavu wakiwemo wanafunzi sambamba na kutenga bajeti kwa ajili ya kuwezesha vyuo kununua vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Kongamano hilo lilishirikisha Watendaji kutoka Idara za Serikali na Taasisi zake, Mashirika na Taasisi zinazotoa huduma kwa watu wenye ulemavu, Walimu, Vyama vya Watu wenye Ulemavu lilitoa fursa kwa washiriki kudadavua masuala mbalimbali ya yanayowahusu wanafunzi wenye Ulemavu na Maendeleo.