…………………………………………………………………………………..
Na Muhammed Khamis TAMWA ZNZ
Wakati Dunia na Tanzania kwa ujumla ikiwa bado katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari Mkuruenzi wa TAMWA-Zanzibar Dkt,Mzuri Issa amesema maadhimisho hayo yanapaswa pia kutazamwa hali ya usawa wa kijinsia kwa wanahabari visiwani hapa kwa kuwa bado wapo baadhi ya wanahabari wanawake wamekua wakikabiliwa na majaribu ya rushwa na ngono wanapoomba ajira.
Aliyasema hato katika mkutano maalumu uliolenga kutazama hali ya uhuru wa habari na umuhimu wa uwepo wa sheria bora ya habari visiwani hapa katika mkutano ulioandaliwa na shirika la Intenrnews Tanzania kupitia mtandao (Zoom)
Alisema hadi sasa vyombo vingi vya habari pande zote mbili za Tanzania hawana sera ya jinsia ambayo wanatumia badala yake hufanya kazi kimazoea na kupelekea wanawake wengi kubaki kuwa nyuma na kukutana na chanagamoto mbali mabali zikiwemo za kudaiwa rushwa ya ngono.
Alisema uwepo wa sera ya jinsia kwenye vyombo vya habari ungeweza kuweka bayana namna gani wanahabri na vyombo vyao wanatakiwa kufanya kazi na wanawake kwa maslahi ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyengine Mkurugenzi huyo alizungumzia kuhusu kukosekana kwa uwajibikaji katika vyombo vingi vya habari zaidi katika suala la mishahara kwa wafanyakazi wao.
Akifafanua zaidi alisema rushwa za ngono hujitokeza zaidi wakati wa ajira kwenye vyombo vya habari na ndipo wasichana wengi hujikuta wanaingia kwenye mtego na wapo wanaoamua kufanya jambo hilo wakiamini ndio njia pekee ya kupata ajira.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha huduma za sharia Zanzibar Harous Mpatani wakati wakati akiwasilisha mada katika mkutano huo aliema haki ya kupata habari ni ya kikatiba na kila anapaswa kupata haki hio bila ya kuminywa.
Alieleza Zanzibar kama sehemu ya dunia imeridhia mikataba ya kimataifa ikiwemo wananchi wake kupata na kutoa habari hawana budi kuheshimu mikataba hio.
Akichangia katika kongamano hilo mwanahabari mwandamizi kutoka Zanzibar Hassan Issa alisema anasikitishwa sana kukosekana kwa umoja katika tasnia hio kiasi ambacho wapo watu Fulani wanaojiona wao bora na kuwaona wengine ni watu wasiokua na maana wakati wote ni wanataaluma sawa.
Alisema tabia za kusemana vibaya na wakati mwengine hata mtu au watu kuwaandalia wenzao mabaya si jambo zuri na linapaswa kuachwa kwa maslahi ya taaluma hio na watu kurudi kuwa kitu kimoja.
Wakati akifunga mdahalo huo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Khamis Abdalla Said amesema ili mabadiliko katika sekta ya habari yaweze kutokea hakuna budi kuwepo kwa umoja kwa wanadao wote na Serikali.
Alisema suala la umoja na mshikamano ni jambo zuri katika kila sehemu na kutokubali kugawiwa wao wenyewe watajikuta wakiwa katika kufanikisha mipango yao pasipo na kutoa malalamiko.
Sambamba na hayo alisema wizara imetakiwa kuzifanyia mapitio baadhi ya sheria na kuwataka waandishi wa habari habari kupeleka mapendekezo yao kwa sheria ambazo wanaziona ni kandamizi kwao.
“Kwa ukweli kabisa ni kwamba Serikali imesikia kilio chenu na ndio maana ikatoa ruhsa mulete mapendekezo ya sera kwa lengo la kupata sharia bora ya habari ambayo italeta manufaa kwa pande zote mbili” alisema.
Hata hivyo alisema pamoja na kuwepo kwa changamoto za kisheria lakini haiwezekani kuachiwa watu kufanya wanavyotaka kwa kuwa kila uhuru una mipaka yake.
Alifahamisha kwamba ni wakati sasa wakaitumia hiyo fursa ya wadau hao wa habari kuziainisha sheria ambazo wanaona zinahitaji kufanyiwa marekebisho badala ya kukaa tu na kulalalamika.