Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga akidadavua kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, kupitia Kituo cha Runinga cha Channel 10, Mei 6, mwaka huu.
Baadhi ya nyumba zilizounganishiwa umeme mkoani Ruvuma kupitia miradi ya umeme vijijini. Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga amesema lengo la Serikali ni kufikisha umeme kwa wananchi wote. Alisema hayo kupitia Kituo cha Runinga cha Channel 10, Mei 6, mwaka huu.
Mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu ya jua. Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga ameeleza kuwa Serikali inaendelea kupeleka umeme katika visiwa vilivyopo nchini kwa kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo ya umeme jua. Alisema hayo kupitia Kituo cha Runinga cha Channel 10, Mei 6, mwaka huu.
Mmoja wa waajiriwa katika kiwanda cha kutengeneza transfoma na nyaya za umeme, kinachomilikiwa na kampuni ya Europe Inc. Industries LTD (TROPICAL) kilichopo jijini Dar es Salaam, Farida Karim akiwa kazini. Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga ameeleza kuwa uanzishwaji wa viwanda vya kuzalisha vifaa vya umeme nchini umeleta manufaa makubwa katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, hususani kutokana na kupungua kwa gharama. Alisema hayo kupitia Kituo cha Runinga cha Channel 10, Mei 6, mwaka huu.
********************
Na Veronica Simba – REA
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga amewataka wakazi wa vijijini ambao maeneo yao hayakufikishiwa umeme baada ya miundombinu yake kufikishwa katika vijiji husika, kuondoa hofu kwani watapelekewa nishati hiyo kupitia Mradi wa Ujazilizi ambao ulishaanza kutekelezwa.
Alitoa ufafanuzi huo wakati akizungumza kupitia Kipindi cha Sema Kweli kilichorushwa na Kituo cha Runinga cha Channel Ten, Mei 6, 2021.
Alisema, Serikali ilibuni Mradi wa Ujazilizi ili kwenda kujazia maeneo ambayo yamefikiwa na miundombinu ya umeme lakini nishati hiyo haijasambaa eneo zima ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma hiyo muhimu.
“Sasa hivi ukienda vijijini, utakuta malalamiko ya baadhi ya wananchi kuwa umeme umefika kwenye kijiji lakini umepelekwa katika taasisi kadhaa kama vile shule na zahanati huku maeneo mengine yakirukwa. Jambo la msingi ni kuwa tumekwishafikisha miundombinu ambayo ni gharama zaidi kuiweka, sasa tunatekeleza miradi ya kujazia umeme vitongoji vyote, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi,” alisisitiza.
Kuhusu kupeleka umeme katika visiwa, Mhandisi Maganga alieleza kuwa, Serikali kupitia REA inaendelea kuvipelekea umeme visiwa vyote nchini kwa kutumia teknolojia mbalimbali zikiwemo za umeme jua na upepo.
Alisema kuwa jumla ya visiwa 72 hadi sasa vimekwishapelekewa umeme kati ya 196 vilivyopo nchini. Aliongeza kuwa mpango unaoendelea kutekelezwa ni kuviunganishia umeme visiwa vingine takribani 53 ambavyo vina makazi ya kudumu ya watu huku akibainisha kuwa vilivyosalia ni vile ambavyo havikaliwi na watu.
“Visiwa 36 kati ya 53 vitaanza kupelekewa umeme kuanzia Julai mwaka huu na vitakavyosalia vitapelekewa katika bajeti ijayo,” alieleza.
Akizungumzia namna ambavyo sekta ya umeme vijijini ilivyonufaika na Mpango wa Serikali wa Uchumi wa Viwanda, alisema uhamasishaji huo wa Serikali umechochea wananchi wengi kuanzisha viwanda vinavyotengeneza vifaa mbalimbali vya umeme hivyo kuwezesha upatikanaji wake hapa nchini.
Alisema, kabla ya kuanzishwa viwanda hivyo, Serikali ilikuwa inalazimika kuagiza vifaa kama nguzo, nyaya, mita na vingine vya aina hiyo kutoka nje ya nchi ambapo ilitumia fedha nyingi tofauti na hivi sasa ambapo utekelezaji wa miradi ya umeme unatumia vifaa vya ndani ya nchi.
“Badala ya kutumia gharama kubwa (takribani asilimia 80) kununua vifaa nje na kunufaisha nchi hizo, sasa vifaa hivyo vinapatikana ndani ya nchi na fedha inabaki nchini. Hayo ni mafanikio makubwa,” alibainisha.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Maganga alieleza kuwa Tanzania iliamua kuchukua mwelekeo tofauti na nchi nyingine zinazotekeleza miradi ya umeme vijijini, ambao wengi wao hupeleka nishati hiyo katika vijiji vilivyo na wakazi wengi wanaotekeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi, wakiamini kuwa ndiyo wenye uhitaji mkubwa.
“Sisi Tanzania tumesema hivi, siyo kwamba mahitaji ya wananchi kule ndiyo yalete nishati bora. Sisi tumesema tupeleke nishati bora ili wananchi wapate maendeleo. Hivyo, tunapeleka umeme kwa wananchi ili uwe kichocheo cha wao kuanzisha miradi ya kiuchumi ambayo itawaletea maendeleo. Ndiyo maana hatuchagui nyumba,” alifafanua.
Katika Kipindi hicho, Mhandisi Maganga alikuwa akizungumzia utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, ambao unaendelea nchini, ambapo sasa umeingia katika Mzunguko wa Pili baada ya kukamilika kwa Mzunguko wa Kwanza.