*******************
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo imeandaa Kongamano la Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika ikiwa ni hatua ya kutambua mchango wa Tanzania katika Ukombozi wa Bara hilo ambalo litaambatana na Siku ya Uanuai wa Utamaduni Dunani.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha Redio cha Dodoma FM kupitia kipindi cha “Kapu Kubwa”, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni, Dkt. Emmanuel Temu ameelezea jinsi Wizara ilivyojipanga kufanikisha maadhimisho hayo ambayo yanatarajia kufanyika Mei 21, 2021 Jijini Dar es Salaam.
“Maadhimisho haya yameanza kufanywa kidunia tangu mwaka 2001 ambapo mwaka huu Wizara kupitia Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika imeandaa kongamano litakalokusanya fikra za wanamajumui wa Afrika kujadili kwa kina mchango wa Tanzania kwenye Ukombozi wa Bara la hili” amesema Dkt.Temu.
Dkt.Temu amefafanua kuwa kongamano hilo linaloongozwa na kaulimbiu ya “Urithi wa Ukombozi Fahari ya Afrika” ni fursa muhimu ya kuwaleta pamoja wanazuoni na wadau wote wa utamaduni kujadili mustakabali wa harakati hizo ili kuendelea kuhifadhi historia ya harakati hizo kwa faida ya vizazi vya sasa na baadae.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini, Yusufu Singo alipofanya mahojiano na Kituo cha Redio cha A FM cha Jijini Dodoma amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Vyombo vya Habari ili kunogesha Michezo hapa nchini.
“Habari na Michezo ni Sekta zinazotegemeana sana kwa mfano mwisho wa juma hili tuna mechi ya Simba na Yanga, bila umma kuelezwa vizuri juu ya mechi hii inaweza kukosa msisimko” amesisitiza Mkurugenzi Singo.
Pamoja na kongamano hilo pia kutakuwa na kikao kazi cha Maafisa Utamaduni na Maafisa Michezo wote nchini kinachoandaliwa na kuratibiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo kitakachofanyika kuanzia Mei 21 hadi 23, 2021 kitakachofanyika Jijini Dar es salaam.