****************************
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU – Brig Jen. John Mbungo, napenda kuujulisha umma kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU – Makao Makuu, imekuwa ikifanya uchunguzi dhidi ya baadhi ya Viongozi wa Chama cha Waalimu Tanzania (CWT) kwa makosa mbalimbali yanayoangukia chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.
Viongozi hao, ambao wanatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka yao kinyume na Kif. cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007 pamoja na Uchepushaji – Kinyume na Kif cha 29 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007 ni hawa wawili wafuatao:
- Deus Gracewell Seif (Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania CWT)
- Abubakar S. Allawi (Mweka Hazina wa Chama cha Walimu Tanzania CWT)
Watuhumiwa hawa, walikuwa wakichunguzwa kwa kosa la uchepushaji pamoja na kutumia madaraka yao vibaya, kama viongozi wa Chama cha Waalimu Tanzania.
Uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ulibaini kwamba mwaka 2018, viongozi hawa walitumia zaidi ya Shilingi Milioni 13.9 mali ya chama hicho, kwa ajili ya kulipia tiketi za ndege pamoja na kulipia gharama za malazi, kwa safari ya kwenda Cape Verde.
Kwa wakati huo – yaani mwaka 2018, Cape Verde kulikuwa na Mechi ya Mpira wa Miguu kati ya Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), waliokuwa wakicheza na Timu ya Taifa ya Cape Verde.
Kwa kufanya hivyo, watuhumiwa hawa wameenda kinyume na vifungu vya 29 pamoja na 31 vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.
Uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU Makao Makuu dhidi ya tuhuma hii umekamilika na hivyo, kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, leo Jumatatu – Mei 3, 2021 watuhumiwa hawa watafikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu – Jijini Dar Es Salaam, ili kujibu mashitaka yanayowakabili.