*********************************
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
RAIS wa New Covenant Unity International (NCUI) ambaye pia ni Kiongozi wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Dkt.Joshua Aram Mwantyala amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa utaratibu wake wa kuendelea kuwafuturisha wananchi mbalimbali kisiwani Unguja na Pemba katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Nabii Dkt.Joshua ameyasema hayo muda mfupi baada ya kutoka katika mlima wa maombi Mjini Morogoro, baada ya kuhitimisha maombi maalum kwa Rais Dkt. Mwinyi ambayo aliyaendesha kwa ajili ya kumuombea Rais Dkt. Mwinyi ili Mungu azidi kumpa nguvu na afya njema aweze kukamilisha kwa wakati malengo yake ya kuifanya Zanzibar kusonga mbele katika nyanja zote.
“Nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi, ni miongoni mwa viongozi wanyenyekevu, wenye hofu ya Mungu, anayesikiliza na kuyafanyia kazi yale ambayo yananufaisha wananchi wote. Utaratibu wake wa kufuturisha makundi mbalimbali ya wananchi ni ibada kubwa sana. Mungu azidi kumpa nguvu na afya tele. Hakika yajayo Zanzibar ni neema tupu,” amesema Nabii Dkt.Joshua.
Amesema, katika maombi hayo Mungu amemuonyesha mambo mengi ya neema na mafanikio ambayo yanakwenda kutokea Zanzibar chini ya Rais Dkt.Mwinyi.
“Hivyo ni ombi langu kwa wananchi, aendelee kumuombea Rais Dkt.Mwinyi na wasaidizi wake, wafanye kazi kwa bidii na walipe kodi halali kwa mamlaka husika kwa wakati, kwani neema hizo zinakwenda kugusa makundi yote kuanzia kukua kwa uchumi na kustawi kwa sekta nyingine,”amesema Nabii Dkt.Joshua.
Awali Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa kisiwani Pemba wakati akifuturishaa wananchi Mkoa wa Kaskazini Pemba alieleza kwamba kitendo cha kufutarisha ni utamaduni uliopo wa viongozi wakuu wa Zanzibar ambao ameamua kuuendeleza.
Hafla hiyo ya futari iliyoandaliwa na Rais Dkt. Mwinyi kwa ajili ya wananchi wa Mkoa huo wa Kaskazini Pemba ilifanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Wete, Pemba ambayo ilihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Serikali, dini, vyama vya siasa pamoja na makundi maalum ya wananchi wa mkoa huo.