Chuo hicho ambacho kilifungwa mwaka 2010 kutokana na changamoto ya ukosefu wa walimu, fedha za uendeshaji, uchakavu wa miundombinu na uhaba wa wanafunzi, kimefunguliwa hivi karibuni.
Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Harieth Mcharo, alisema chuo hicho kilichofunguliwa mwaka 1998 kinatoa mafunzo ya fani za umeme wa majumbani, ushonaji nguo na ubunifu,uchomeleaji vyuma, useremala kinakabiliwa na tatizo la maji na uchakavu wa miundombinu ya maji, mabaweni na vyoo.
“Chuo hiki kilisimama mwaka 2010 sababu ya ukosefu wa walimu,wengine walistaafu,ugonjwa na vifo pamoja na uhaba wa wanafunzi ila kwa sasa tumepata mfadhili ametuchimbia kisima cha maji na amekarabati vyoo vya nje,”alisema Mcharo.
Alisema chuo hicho baada ya kufunguliwa tena kimepokea wanafunzi 30 kupitia kwa wadau mbalimbali ambapo wanafunza 24 wamefadhiliwa na taasisi ya The Desk & Chair Foundation.
Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, Alhaji Sibtain Meghjee alisema kutokana na chuo hicho kutokuwa na uwezo wa kulipa Ankara ya matumizi ya maji, imewachimbia kisima cha maji.
Alisema watauomba uongozi wa maabara ya maji kupima sampuli ya maji hayo kuona kama yanafaa kwa matumizi ya binadamu ili yatumiwe na wanafunzi na kukipunguzia chuo mzigo wa gharama.
Aidha aliahidi kufunga pampu ya kusukuma maji hadi kwenye tenki la kuhifadhi maji na itaboresha mfumo wa usambazaji maji chuoni hapo.