****************************
Na Mwandishi wetu, Babati
KLABU ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Manyara (MPC) imeadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani kwa kutoa msaada wa vyakula kwa kituo cha watoto cha MAHOCE na kituo cha wazee cha Magugu (Sarame) Wilayani Babati.
Mwenyekiti wa MPC Zacharia Mtigandi akizungumza mjini Babati amesema wametoa msaada huo ili kushiriki pamoja madhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari na watoto na wazee hao na kuzindua blog itakayotumiwa na wanachama hao.
Mtigandi amesema kwenye kituo cha watoto cha Manyara holistic centre (MAHOCE) waliwapatia mchele kilo 100, mafuta ya kupikia lita 20 na mifuko miwili ya lawalawa.
Amesema kwenye kituo cha wazee Magugu (Sarame) waliwapa mchele kilo 50, lita 20 za mafuta na kunywa sharubati pamoja na wazee hao.
Amesema MPC iliamua kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani kwa kushiriki na watoto na wazee hao badala ya wadau wengine wa habari.
“Pia tumezindua blog ya chama ambayo waandishi wa habari watakuwa wanaitumia kwa lengo la kuchakata habari hasa za vijijini hivyo watumie fursa hiyo kwa kuandika habari nyingi zaidi za kijamii,” amesema Mtigandi.
Mkurugenzi wa MAHOCE Joshua Johnson amewashukuru waandishi hao wa habari kwa kuwatembelea na kuwapa msaada huo wa vyakula kwenye madhimisho hayo ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari.
Amesema kituo hicho kilianzishwa mwaka 2007 na kina watoto 80 kinaowahudumia japokuwa changamoto ya barua nyingi wanapata wakiombwa kuhudumia watoto wengi zaidi ya hao.
Mmoja kati ya waandishi wa habari wanachama wa MPC, Mohamed Hamad amesema amefurahishwa na namna waandishi wa walivyojumuika katika madhimisho hayo.
“Tumetembelea kituo cha watoto cha MAHOCE, kituo cha wazee Magugu cha Sarame na kuzindua blog ya chama ambayo itakuwa inafanyiwa kazi na waandishi wa habari wanachama wa klabu yetu,” amesema.
Makamu Mwenyekiti wa MPC, Mary Margwe amesema kwa kipindi hiki wameadhimisha tofauti na miaka iliyopita ambapo walikuwa wanakutana na wadau mbalimbali wa habari wa mkoa huo.
“Tulikuwa tunakutana na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na viongozi mbalimbali wa taasisi tofauti za Mkoa wa Manyara ila mwaka huu imekuwa tofauti,” amesema Margwe.