Mkuu wa Mkoa wa kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti akiongea na Viongozi wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri wakati wa kikao kazi cha uraghibishaji na uhamasishaji wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi Kipaumbele kwenye Mkoa huo ambacho kiliwajumlisha Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa halmashauri,Waganga Wakuu wa Wilaya, Maofisa Elimu wa halmashauri pamoja na waratibu wa magonjwa Yaliyokuwa hayapwi Kipaumbele kwenye Hamashauri hizo.
Wakuu wa Wilaya na washiriki wengine wa Mkoa wa Kagera wakifuatilia mada zilizotolewa na wawasilishaji kutoka Mpango wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mwakilishi wa Mratibu wa Taifa wa Mpango wa Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Bw. Oscor Kaitaba akiwasilisha mada kwenye kikao kazi hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Gaguti akifuatilia mada zilizowasilishwa kwenye kikao kazi hicho kilichowakutanisha Viongozi kutoka halmashauri nane za mkoa wa Kagera.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Prof. Faustine Kamzola akiongea wakati wa kikao kazi hicho ambapo aliwasisitiza viongozi wa dini kusaidia kutoa elimu kwa waumini wao umuhimu wa kinga ili kuwa na afya njema
Na. Catherine Sungura,WAMJW,Kagera
Viongozi wa ngazi ya Mkoa, Wilaya na Halmashauri wametakiwa kuwahamasisha wananchi kwenye maeneo yao husuan kwenye kupambana na kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kwani changamoto zozote za afya zinaathiri moja kwa moja uchumi.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti wakati wa kikao kazi cha uraghibishaji na uhamasishaji wa Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTD) kwa viongozi wa Mkoa,Wilaya na halmashauri zote za Kagera kilichoandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa hayapewi Kipaumbele.
“Changamoto zozote za afya zina athiri moja kwa moja uchumi, kama sisi viongozi tusipokuwa na afya hatutoweza kutoa huduma kwa usahihi kwa watu tuliopewa dhamana ya kuwasimamia maendeleo yao”.
Aliongeza kuwa kama jamii inakwazwa kwa njia moja au nyingine inaathiri muda wa wananchi na utoaji wa nguvu zao kwenye tija ya kazi wanazozifanya kwani magonjwa hayo kwa watu wazima hawayaoni kama ni ajenda muhimu bali wamekuwa wakipigania kwa watoto chini ya miaka mitano.
“Sisi watu wazima hatuoni kama ni ajenda muhimu kupambana na magonjwa haya na tumekuwa tunapigania kwa watoto chini ya miaka mitano,niendelee kutoa msisitizo kwa wana Kagera kuona umuhimu wa kuunga mkono jitihatazda za Serikali kwa watanzania kuwa wenye afya njema kwani wanatoa mchango mkubwa kwenye kazi zetu zinafikiwa”.
Hata hiyo Mkuu huyo wa mkoa aliwataka viongozi wa mkoa huo kuendelea kushirikiana na wadau wote na endapo wadau hao wataondoka basi mkoa utasimama wenyewe na hivyo kuwataka kutenga bajeti za fedha za ndani za kupambana na magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele na yale mengine ambayo yanaathiri shughuli za utendaji wa kila siku.
Aidha, Mhe. Gaguti amewataka viongozi hao kuimarisha elimu ya afya pamoja na usimamizi wa kusimamia afya kwa kufanya ukaguzi kwenye maeneo yote ya huduma za kijamii pamoja na makazi ya wananchi kwa kuzingatia usafi wa mazingira pamoja na unawaji wa mikono .
Amesema udhibiti wa magonjwa kwa wananchi itakuwa na manufaa makubwa kwa kuishi maisha marefu,na kuepuka matumizi ya dawa ya mara kwa mara na pia kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi kwa kujikinga na maradhi hayo.
Hata hivyo ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuandaa kikao kazi hicho kwani kama mkoa wamekuwa wakitekeleza jitihada za kupambana na kudhibiti magonjwa mbalimbali hivyo kwa magonjwa hayo ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele ni muhimu sana katika kupigania afya za watanzania.
Naye Mwakilishi wa Mratibu wa Taifa wa Mpango wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele Wizara ya Afya Bw.Oscar Kaitaba amesema kama mpango wana lengo la kuwawezesha wananchi kuwa na afya bora na kwa mkoa wa kagera wanatoa kinga tiba ya kichocho na minyoo ya tumbo kwa watoto wenye umri wa kwenda shule (walioandikishwa na wasioandikishwa) kuanzia miaka 5 hadi 14.
Wakati huo huo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Dkt. Issessanda Kaniki amesema zoezi la ugawaji kinga tiba linahitajika sana kwenye mkoa huo katika halmashauri zote nane na hivyo mkoa umejipanga kutekeleza zoezi hilo kwa uhamasishaji kuanzia ngazi ya viongozi na jamii .
Dkt. kaniki amesema kwa upande wa usafi wa mazingira amesisitiza wananchi kuzingatia usafi wa mazingira kwenye maeneo yao ya makazi pamoja na vituo vyote vya kutolea huduma za kijamii ili kuepuka na magonjwa yanayosababishwa na uchafu na kuwataka wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya vyoo, kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni na kuzingatia lishe bora ili kuepuka na magonjwa.