Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya kwa ajili ya ziara ya siku mbili
Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akiwasalimia baadhi ya Wafanyabiashara wa Tanzania waliopo nchini Kenya alipowasili jijini Nairobi kwa ziara rasmi ya siku mbili nchini Kenya. |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi nchini Kenya kuanza ziara rasmi ya siku mbili kufuatia mwaliko wa mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta.
Alipowasili jijini Nairobi Mhe. Rais Samia alilakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Raychelle Omamo na Waziri wa Michezo, Utamaduni na Urithi Mhe. Amina Mohammed.
Baada ya kuwasili Mhe. Rais Samia aliekea hotelini kwa ajili ya mapumziko kidogo na baadaye alielekea Ikulu ya Nairobi kwa ajili ya kupokelewa rasmi na Mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta ambapo alikagua gwaride na kupigiwa mizinga 21 kwa heshima yake.
Akiwa Ikulu jijini Nairobi Mhe. Rais alifanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake Mhe. Rais Kenyatta na baadaye walifanya mazungumzo rasmi ambayo yalihudhuriwa na wajumbe wa pande zote mbili.
Baada ya kumaliza mazungumzo yao viongoazi hao walizungumza na waandishi wa habari na baadaye Mhe. Rais Samia alikwenda kuweka shada la maua katika Kaburi la Baba wa Taifa la Kenya hayati Mzee Jomo Kenyatta.
Jioni Mhe. Rais atahudhuria dhifa ya Kitaifa ambayo imeandaliwa kwa heshima yake na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta.
Kesho tarehe 05/05/2021 Mhe. Rais akiwa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta atahutubia Mabunge ya Kenya na baadaye atafungua Kongamano la wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania linalofanyika jijini Nairobi.
Mhe. Rais anatarajiwa kurejea nyumbani siku hiyohiyo ya tarehe 05/-05/2021