**********************************
LEO Mei 3, 2021, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na wadau wote duniani kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.
Siku hii ya kimataifa ilitangazwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Disemba 1993, kufuatia pendekezo la Mkutano Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO). Tangu wakati huo, kila ifikapo tarehe 3 Mei dunia imekuwa ikiadhimisha siku hii ya Uhuru wa Vyombo vya Habari.
Lengo la kuwepo kwa siku hii ni kuenzi uwepo wa misingi ya uhuru wa vyombo vya habari, kutathmini na kuangalia namna bora ya kuulinda uhuru huo ili uendelee kuwepo na kuwakumbuka waandishi wa habari waliopoteza maisha yao wakati wakitekeleza wajibu wao.
Ujumbe wa maadhimisho ya mwaka huu ni: “Habari kwa Manufaa ya Umma” (Information as a Public Good). Ujumbe huu unatoa majukumu mazito kwa watendaji katika tasnia ya habari, Serikali na wadau wengine kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinatumika vizuri ili vitoe matokeo mazuri yanayochochea amani, utulivu, umoja, na mshikamano, hivyo kuwawezesha wananchi na Taifa kwa ujumla kupata maendeleo endelevu.
Tume ya Haki za Binadamu na utawala Bora inazishukuru Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuweka mazingira yaliyoiwezesha Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki kuwa na vyombo vingi zaidi vya habari; ukiwa ni mwelekeo chanya katika kuheshimu na kudumisha uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na haki ya kupata taarifa.
Pia Tume inaishukuru na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utashi wa kisiasa iliouonesha hivi karibuni wa kuvifungulia vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa kwa muda mrefu. Ni matumaini ya Tume kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa habari kwa kuimarisha usimamizi na kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa tasnia ya habari nchini.
Kwa muktadha huo huo, THBUB inapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini kwa kuchangia maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla kwa kuandika na kusambaza habari zinazoelimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo afya, uchumi, siasa, mazingira, michezo na burudani kutaja japo kwa uchache. Pamoja na mafanikio yaliyopo, tasnia ya habari hapa nchini inakabiliwa na changamoto kadhaa katika utekelezaji wa majukumu yake. Miongoni mwa changamoto hizo ni: uwepo wa mapungufu katika baadhi ya vifungu vya sheria, na kuporomoka kwa maadili na weledi kwa baadhi ya waandishi wa habari.
Hivi karibuni kumeshuhudiwa baadhi ya vyombo vya habari na wanahabari kushindwa kuzingatia maadili na misingi ya taaluma ya uandishi wa habari kwa kuandika na kusambaza taarifa za uzushi, kashfa, chuki na uchochezi zenye viashiria vya kuvuruga amani na mtangamano wa Taifa.
Ni wito wa Tume kuwa ujumbe wa maadhimisho ya mwaka huu, wa “Habari kwa Manufaa ya Umma” uwakumbushe wanahabari na vyombo vya habari kuwa habari nzuri na bora ni zile zinazogusa na kuufaidisha umma, na zinazotambua, kulinda na kuendeleza ustawi wa umma kwa ujumla.
Jukumu la kuifanya tasnia ya habari iheshimike na iwe na mchango wenye tija kwa jamii na Taifa kwa ujumla ni jukumu letu sote; yaani mtu mmoja mmoja, tasnia ya habari, jamii, Serikali, asasi za kiraia na sekta binafsi. Hata hivyo, wajibu mkubwa bado unabakia kwa vyombo vya habari na wanahabari, iwapo watawajibika ipasavyo na wakizingatia sheria, weledi, maadili ya kitaaluma na haki.
Ili kuifanya tasnia ya habari kuwa na mchango wenye tija kwa Taifa Tume inatoa wito ufuatao kwa wadau:
- Serikali
- Iendelee kusimamia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza tasnia ya habari.
- Ikae na wadau husika ili kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo.
- Iweke mazingira wezeshi kwa vyombo vya habari kuwa hai, ikiwemo kuvipatia matangazo kwa kuzingatia vigezo vya kimasoko.
- Vyombo vya habari na wanahabari
- Watambue wajibu wao na kuzingatia, sheria, weledi na maadili ya kitaaluma yanayoiongoza tasnia ya habari.
- Watumie mifumo na taratibu zilizowekwa kudai na kushawishi mabadiliko ya sheria zinazoashiria kuminya uhuru wa vyombo vya habari.
- Watambue kuwa kila penye uhuru na haki, pia kuna wajibu. Hivyo vyombo vya habari vitambue kuwa vina wajibu wa kuhabarisha jamii, kuelimisha na kuburudisha, kwa kuzingatia sheria, weledi, maadili, na ukweli.
- Wanahabari wawe wazalendo wa kweli na waipende nchi yao.
- Wanasiasa
- Watambue nafasi na wajibu wa vyombo vya habari kwa maendeleo ya Taifa.
- Wananchi
- Waepuke kusambaza taarifa ambazo vyanzo vyake havina uhakika na zinazoweza kupelekea uvunjifu wa amani na ukosefu wa mtangamano.
- Wazingatie sheria zinazohusiana na tasnia ya habari.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inawahakikishia wadau wa habari kuwa itaendelea kulinda, kukuza na kutetea haki za binadamu nchini, na itaendelea kupaza sauti na kukemea uvunjwaji wa haki ya uhuru wa kujieleza, kutoa maoni na kupata habari na haki nyinginezo kwa wadau.