…………………………………………………………………………………………..
Na.Faustine Gimu Galafoni ,Kahama
Boma la zahanati kijiji cha Sungamile ujenzi ulioanza mwaka 2005 na kukamilisha boma mwaka 2014 kwa nguvu na michango ya wananchi likisubiria kumaliziwa na serikali sehemu ya paa.
Wananchi wa kijiji cha sungamile kata ya mwalugulu halmashauri ya msalala wilayani kahama mkoani shinyanga wameiomba serikali kukamilisha boma la zahanati la kijiji hicho walilojenga kwa nguvu zao wenyewe tangu mwaka 2014.
Wakizungumza na mtandao huu kwa nyakati tofauti hivi karibuni baadhi ya Wananchi hao walisema ni takribani zaidi ya miaka 7 sasa tangu wakamilishe boma la zahanati ,hvyo wameiomba serikali kukamilisha boma hilo hili wapate huduma za afya karibu kwani walikamilisha ujenzi waboma la zahanati pamoja na boma la nyumba ya mganga kwa nguvu zao wenyewe tangu mwaka 2014 na kilichobaki ni ukamilishaji wa kuezeka paa kwa upande wa serikali.
Mipawa Busumabu ni mmoja wa wakazi wa kijiji hicho ambapo alisema walishachanga kwa ajili ya ujenzi wa boma la zahanati lakini hadi sasa halijaezekwa na hawajui hatma ya zahanati hiyo.
“Hatujui hatma ya zahanati katika kijiji chetu ,hatuna zahanati na tunatembea umbali mrefu zaidi ya kilometa 8 hadi 9 kufuata huduma za afya tunaomba serikali itufikirie”alisema.
Ally Daud ,Bi.Nshoma Mlyasele ,Ibrahim Jilumba pamoja Limi Bungu walisema kuna madhara makubwa kwa jamii ya kijiji hicho kutokuwa na huduma ya afya ikiwa ni pamoja na madhara ya uwezekano wa vifo kwa akina mama wajawazito na wagonjwa hivyo kuna haja kubwa ya kuwa na huduma ya afya kijijini Sungamile.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Sungamile Wilayani Kahama mkoani Shinyanga Dulla Pascal Maziku alisema kuwa walianza mchakato wa kuchangisha kwa Tsh.elfu 10 kwa kila kaya na mifuko ya saruji mwaka 2005 na hatua za ujenzi zikaendelea na kufikia mwaka 2014 walikamilisha boma la zahanati na nyumba ya mganga na wanasubiria mpaka leo serikali ikamilishe kuezeka.
“Mimi kama mwenyekiti wa kitongoji tulikaa na halmashauri ya kijiji namna ya kuchangisha na wananchi waliitikia kwa nguvu zote wakajitolea katika ujenzi huo lakini mpaka sasa nyasi ,vichaka vimeanza kuota ndani ya jengo hilo limekuwa likinyeshewa na mvua nyakati za masika tofali zinaharibika”alisema.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mwalugulu ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala Flora SagaSaga amesema kuwa kwa mwaka huu wa fedha halmashauri ya Msalala imepatiwa Milioni 150 kutoka serikali kuu huku boma la zahanati ya Sungamile likiwa kwenye mpango wa fedha za CSR kutoka mgodini.
“Msalala tuna maboma mengi kwelikweli , kata yangu ina zahanati 1 ,vijiji 6 na ina maboma 5, hivyo uhitaji wa zahanati ni mkubwa , kila mwaka tunatoa kidogokidogo kwa mwaka huu tumeletewa Milioni 150 kila zahanati kwa zahanati 3 na katika zahanati ya Sungamile tumeshapata fedha za CSR kutoka mgodini wakati wowote tunaweza kuanza kumalizia hiyo zahanati ,wananchi Sungamile waamini sasa kuwa hiyo zahanati inaenda kuisha”amesema
Mhe.Flora Sagasaga Diwani kata ya Mwalugulu na makamu mwenyekiti Halmashauri ya Msalala Kahama Shinyanga.
Aidha,Makamu mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya Msalala amesema hatua za awali wataanzia katika Zahanati za Mwankima ambapo boma la zahanati hiyo lina takribani miaka 15 hadi sasa huku ukarabati wa zahanati ya kata ya Mwalugugulu ukiwa umekamilika na fedha za ndani za halmshauri zilizopatikana ni milioni 17.5 kufikia mwezi wa sita mwaka huu huduma za afya zitaanza kutolewa Mwankima.
Katika hotuba ya Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa[TAMISEMI] Ummy Mwalimu akiwasilisha Bungeni jijini Dodoma hivi karibuni makadirio ya mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2021/2022 alisema kwa mwaka wa fedha 2020/2021 serikali ilitenga Tsh.Bilioni 27.75 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati 555 ikiwa ni wastani wa maboma 3 kwa kila halmashauri .