………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti amewataka wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule ya msingi Tanzanite ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha wanafunzi wanakula chakula cha mchana shuleni hapo.
Mkirikiti ameyasema hayo alipofanya ziara ya kutembelea shule hiyo na kukagua ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na matundu saba ya vyoo.
Amesema wazazi na walezi wa shule hiyo wanapaswa kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa wanafunzi hao kwani serikali imeshatekeleza wajibu wake kupitia elimu bila malipo.
“Chakula wanachokula nyumbani hawa wanafunzi ndicho hicho ambacho wanakula shuleni, hivyo wazazi na walezi wahakikishe wanatekeleza wajibu wao kwani sisi serikali tumeshatimiza majukumu yetu,” amesema Mkirikiti.
Amesema wazazi na walezi ambao watakuwa kikwazo cha kutimiza hilo apewe taarifa zao ili aweze kuwachukulia hatua kwani wanafunzi wanapokuwa wanakula shuleni kiwango cha taaluma huongezeka.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Tanzanite, Anociatha Salla akisoma taarifa ya shule hiyo amesema ina wanafunzi 1,016 wakiwemo wavulana 518 na wasichana 498 wakitumia vyumba sita kwa uwiano wa wanafunzi 169 kwa chumba kimoja cha darasa.
Mwalimu Salla amesema kwa mujibu wa sera ya mwaka 1995 inaelekeza chumba kimoja kwa wanafunzi 45 ila vyumba viwili vinavyojengwa vitapunguza kwa kiasi changamoto ya madarasa.
“Tunapongeza jitihada za mheshimiwa diwani wa kata ya Mirerani Salome Mnyawi na nguvu za wananchi kujenga vyumba viwili vya madarasa na serikali kumaliza na pia tunaanza msingi wa madarasa mengine,” amesema mwalimu Salla.