Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Dk. Seleman Serera, akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Makutupa wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ambaye alikwenda kuwasha umeme kwenye Kijiji hicho.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Makutupa wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma kabla ya kuwasha umeme kwenye Kijiji hicho.
Baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Makutupa wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) wakati akizungumza nao kabla ya kuwasha umeme kwenye Kijiji hicho.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwahamasisha wananchi wa Kijiji cha Makutupa kilichopo Kongwa kutumia kifaa ‘UMETA’ ili kupunguza gharama za kuunganisha mfumo wa umeme majumbani.
Waziri wa Nishati, Dkt,Medard Kalemani akikata utepe ikiwa ni ishara ya kuwasha umeme katika Kijiji cha Makutupa, wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma. wa kwa kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Suleiman Serera.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa eneo la Mbande, wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma mara baada ya kutoka kuwasha umeme katika kijiji cha Makutupa.
………………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Kongwa
Serikali imesema inatekeleza miradi ipatayo minne ya umeme katika Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kuhakikisha maeneo yote yanapata umeme na kuwawezesha wananchi kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi zitakazo wezesha kujikwamua kiuchumi.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Medard Kalemani wakati akiwasha umeme katika kijiji cha Makutupa Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya hiyo na watumishi wa TANESCO.
Amesema endapo miradi hiyo ikikamilika itawezesha Vijiji mbalimbali kupata nishati ya umeme hali itakayosisimua shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma.
Waziri Dkt Kalemani ametaja miradi inayotekelezwa kuwa ni mradi wa kusambaza umeme vijijini unaoendelea sasa wa awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu ijayo, mradi wa kupeleka umeme vitongojini, mradi wa kupeleka umeme kwenye maeneo yaliyo karibu na mitaa mijini (Peri-urban) na miradi inayotekelezwa na TANESCO.
“Kwa Mradi wa kusambaza umeme vijijini Dodoma, Serikali imetoa takriban shilingi bilioni 60, mradi wa kupeleka umeme vitongojini Serikali imetoa shilingi bilioni 48.3, kwa mradi wa Peri-Urban Serikali imetoa shilingi bilioni 23 na mradi mwingine unatekelezwa na fedha kutoka TANESCO kama ilivyo hapa Makutupa.” amesema Dkt.Kalemani
Dkt Kalemani amebainisha kuwa katika kazi ya usambazaji umeme katika vijiji mbalimbali Mkoa wa Dodoma takribani vijiji 467 vimeshasambaziwa umeme, kati ya vijiji 581 vilivyopo ambayo ni zaidi ya asilimia 81 huku akibainisha vijiji vilivyobaki miradi inaendelea.
Dkt Kalemani amebainisha kuwa kwa Wilaya ya Kongwa ni vijiji vinne (4) tu ndivyo havijafikiwa na nishati ya umeme Kati ya vijiji 87 vilivyopo katika Wilaya ya Kongwa ambapo ndani ya miezi mitatu vitafikishiwa umeme.
Pia ameiagiza TANESCO kufungua Ofisi haraka katika Kijiji cha Makutupa ili kurahisisha itoaji wa huduma kwa wateja wanaounganishiwa umeme.
Dkt.Klaemani pia ametembelea eneo la Mbande ambalo wananchi wake wamekuwa wakilalamika kuwa kuna nguzo za umeme zilizosimikwa muda mrefu bila wananchi hao kuunganishiwa umeme.
Akiwa katika eneo hilo, Dkt.Kalemani amewahidi kuwa, Mkandarasi, kampuni ya Derm Electric ataanza kuwaunganishia umeme wananchi kuanzia Ijumaa ya tarehe 7 Mei, 2021.
Akizungumza na wananchi wa Makutupa na Mbande, Dkt.Kalemani amewasisitiza kutumia umeme kwa matumizi mbalimbali kwani Serikali inatumia fedha nyingi kufikisha umeme katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na kupunguza gharama za uunganishaji ili kila mtanzania atumie nishati hiyo muhimu.
Hata hivyo Dkt.Kalemani amepiga marufuku kwa wananchi kununua nguzo za umeme ili wainganishiwe umeme huku akiweka msisitizo wa gharama za kunganishiwa umeme ni shili elfu 27 tu.
Dkt.Kalemani amesema kwa vijiji 1974 ambavyo bado havijasambaziwa umeme kwa nchi nzima kati ya vijiji 12,268, wakandarasi wa kusambaza umeme kwenye vijiji hivyo wameshapatikana na wataingia katika maeneo ya kazi wiki ijayo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Suleiman Serera,amemshukuru Waziri pamoja na Wizara yake kwa kazi ambayo wamekiwa wakiifanya kwa kuwasmbazia wananchi huduma ya umeme ambapo itaimarisha uchumi wao.
”Kama unavyojua katika eneo letu la Dodoma linahitaji sana umeme na wilaya yetu ya Kongwa shughuli nyingi zimefanyika tunavyo vijiji 87 tunaishukuru sana wizara yako vijiji 79 umeme umefika,Vitongoji 384 katika vitongoji hivyo 225 umeme umefika vingine bado”amesema Dkt.Serera.