……………………………………………………………………………………..
Na Damian Kunambi, Njombe.
Halmashauri ya wilaya ya Ludewa iliyopo mkoani Njombe imekusanya zaidi ya bilioni 17 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020-2021 kati ya zaidi ya bilioni 30 zilizokusudiwa kukusanywa katika kipindi hicho cha mwaka wa fedha.
Hayo yamesemwa na mjumbe wa kamati ya fedha, uongozi na mipango pambaye ni diwani wa kata ya Iwela Joachim Lukuwi alipokuwa akisoma taarifa ya kamati hiyo kwa niaba ya mwenyekiti wa kamati Wise Mgina katika kikao cha baraza la madiwani cha robo tatu ya mwaka 2020 – 2021 kuanzia mwezi January hadi March 31 mwaka huu.
Ameongeza kuwa mpaka kufikia March 31 mwaka huu halmashauri hiyo imekwisha tumia asilimia 51.8 ya fedha hizo zilizokusanywa katika miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Aidha kamati hiyo imemtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo Sunday Deogratias kusimamia vyema suala la ukusanyaji mapato sambamba na kumshauri kuwabadilisha baadhi ya watumishi waliopo katika geti la Lusitu ili kuweza kuongeza ufanisi wa kazi katika ukusanyaji mapato.
Wakati huohuo mwenyekiti wa halmashauri hiyo Wise Mgina ambaye pia ni diwani wa Mundindi alimtaka mkurugenzi huyo kusimamia vyema miradi ya maendeleo iliyopo katika kata mbalimbali huku akisisitiza kuonyesha ushirikiano wa kutosha katika miradi inayotekelezwa kwa nguvu za wananchi.
Amesema wananchi wanajitoa sana katika kuanzisha miradi ya maendeleo hasa ujenzi wa zahanati hivyo serikali inapaswa kuonyesha ushirikiano wao kwa kuunga mkono juhudi hizo zinazofanywa na wananchi.
“Mkurugenzi naomba sana hii miradi inayojengwa kwa nguvu za wananchi tuipe kipaumbele katika kukamilisha, wananchi wanatumia nguvu zao kujenga jengo mpaka linamalizika pasipo serikali kuchangia chochote hivyo serikali inapohitajika kukamilisha hatua za mwisho inapaswa kufanya kwa wakati ili kutowakatisha tamaa wananchi hao waliojitoa”, Alisema Mgina.
Aidha kwa upande wa mkurugenzi huyo aliyapokea maagizo hayo na kuwaomba madiwani kutumia kwa wakati fedha za maendeleo zinazofika katika kata zao kwani endapo utekelezaji utacheleweshwa itapelekea fedha hizo kurudishwa hazina.
Deogratias amesema fedha hizo zinaporudishwa hazina kutokana na kutotumika kwa wakati huleta athari kwa halmashauri kwani itaonekana fedha zinazoletwa ni nyingi kuliko uhitaji wetu kitu ambacho si cha kweli.
“Waheshimiwa madiwani itakuwa haileti afya endapo fedha za maendeleo zitarudi hazina itapelekea kupunguziwa fedha katika bajeti ijayo hivyo niwaombe miradi iliyopangwa itekelezwe kwa wakati”. Alisema Deogratias.