*************************
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amekutana na Vyama vya Michezo vinavyosimamia michezo ya Wanawake nchini ili kujadili mbinu mbalimbali za kuinua michezo kwa kundi hilo.
Dkt. Abbasi amekutana na wadau hao leo Aprili 29, 2021 Jijini Dar es salaam ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan la kutaka wanawake kuzingatiwa katika michezo.
“Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa wadau wa michezo, hivyo tunakaribisha mawazo ambayo yatasaidia kuboresha michezo upande wa wanawake, tupate mawazo mapya ya michezo badala ya kujikita kwenye michezo ile ile, Tanzania inaweza kukosa ubingwa wa dunia kwenye mpira wa miguu ila ikatoa bigwa wa dunia kwenye michezo ya jadi” amesema Dkt. Abbasi.
Aidha, Dkt. Abbasi amevishauri vyama hivyo vya michezo nchini kujipanga ili kufanya mashindano ya kitaifa (Taifa Cup) kwa pamoja ili ijulikane hatua itakayosaidia kupata fedha kwa ajili ya kuendesha mashindano hayo.
“Tupange wiki ya mashindano na tuchague michezo yetu maalum itakayochezwa, hii itasaidia kupata fedha kutoka kwa wadau, Serikali na kuitangaza michezo hiyo kwa urahisi. Tuna mashindano mengi ya Taifa lakini hayajulikani kwa sababu kila chama cha michezo kinafanya michezo husika kwa wakati wake” amesema Dkt. Abbasi.
Akizungumza katika kikao hicho Kaimu Katibu wa Riadha Tanzania (RT) Bi. Ombeni Zavara amebainisha changamoto mbalimbali zinazokabili vyama hivyo nchini ikiwemo uhaba wa fedha, ukosefu wa viwanja kwa ajili ya mazoezi, kodi ya vifaa vya michezo ambapo Dkt. Abbasi ameahidi kukutana na kila chama ili kuweza kuzumgumza nao na kutatua changamoto zinazowakabili ili kuimarisha michezo nchini upande wa wanawake.