Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Madaba mkoani Ruvuma Shafi Mpenda akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika kikao cha robo ya tatu ya Baraza la madiwani kilichofanyika jana,katikati mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Theofanes Mlelwa.
Picha na Muhidin Amri
………………………………………………………………………..
Na Muhidin Amri,Madaba
BARAZA la madiwani la Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma,limempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Shafi Mpenda Halmashauri kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo na kazi nzuri ya kusimamia mapato na matumizi ya fedha za Halmashauri.
Wakiongea kwenye kikao cha Baraza la madiwani kilichofanyika jana baadhi ya madiwani walisema,licha ya Halmashauri hiyo kuwa changa na kuwa na vyanzo vichache,hata hivyo Mpenda anafanya kazi nzuri ya kukusanya mapato kutoka kwenye vyanzo vilivyopo.
Diwani wa kata ya Mkongotema Vestus Mfikwa alisema,juhudi zinazofanywa na Mkurugenzi kwa kushirikiana na watumishi wengine wanaofanya kazi ya kukusanya mapato ya ndani usiku na mchana zimewezesha halmashauri hiyo kujiendesha katika shughuli zake.
Diwani wa kata ya Matumbi Valentine Mtemahuti alisema, kazi nzuri ya kusimamia na kukusanya mapato inayofanywa na watumishi imesaidia hata kuboreshwa kwa huduma mbalimbali za kijamii kama afya.
Alitolea mfano kuanzishwa kwa Duka la Dawa katika kituo cha afya Madaba ni kati ya vitu vizuri vilivyotekelezwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri.
Alisema,kumesaidia wananchi hususani wagonjwa wanaofika kwa ajili ya huduma za matibabu kupata dawa kwa bei rahisi ikilinganisha na maduka ya watu binafsi.
Hata hivyo,amemuomba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kuangalia uwezekano wa kuanzisha maduka ya dawa kwenye zahanati zilizopo katika vijiji vya pembezoni ili kuwasaidia wananchi kupata dawa kwa bei nafuu.
Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema licha ya kuipongeza Halmashauri kwa kupata hati safi na juhudi mbalimbali zinazofanywa katika suala zima la kukusanya mapato,ameitaka kufanyia kazi hoja mbalimbali zilizotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG).
Aidha,ameiagiza kuweka mikakati itakayosaidia wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kufanya vizuri na kumaliza tatizo la baadhi ya wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani yao.
Mgema alisema, katika mtihani wa kidato cha pili mwaka jana jumla ya watoto 18 wamepata alama sefuli na wanafunzi 26 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana walipata sefuli.
“ni lazima ifanyike tathimini ya miundombinu ya shule,madarasa,viti,meza na vyoo ili kuondoa tatizo la wanafunzi kufanya vibaya katika mitahani ya kitaifa”alisema Mgema.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Songea Nelly Duwe alisema, Halmashauri ya wilaya Madaba ndiyo inayoibeba wilaya hiyo kwa mambo mengi mazuri ikilinganisha na Halmashauri nyingine,hivyo amewahimiza kuendelea kuchapa kazi na kamwe wasibweteke na mafanikio waliyoyapata.