Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Wakili Richard Odongo, akiwasilisha mada kuhusu Majukumu ya Mamlaka za Nidhamu na Rufaa kwa Walimu kwenye mafunzo ya wajumbe wa Kamati za Wilaya, Kanda ya Ziwa, Aprili 29, 2021 jijini Mwanza.
Wajumbe wa Kamati za Wilaya zinazoshughulikia Ajira na Nidhamu kwa Walimu, wakimsikiliza Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Wakili Richard Odongo, alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu Majukumu ya Mamlaka za Nidhamu na Rufaa kwa Walimu kwenye mafunzo hayo yaliyoshirikisha mikoa ya Kanda ya Ziwa, Aprili 29, 2021 jijini Mwanza.
*****************************
Na Veronica Simba – TSC
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Wakili Richard Odongo, amewaasa wajumbe wa Kamati za Wilaya zinazosimamia Ajira na Maadili ya Walimu, kutenda haki wanaposhughulikia mashauri ya walimu, pasipo kujali mazingira magumu ambayo wakati mwingine yanaweza kuwaathiri wao pia.
Wakili Odongo ametoa wito huo leo Aprili 29, 2021 jijini Mwanza, wakati akiwasilisha mada inayohusu Majukumu ya Mamlaka za Nidhamu na Rufaa kwa Walimu katika mafunzo ya Wajumbe wa Kamati husika za Wilaya, Kanda ya Ziwa.
Akifafanua, ameeleza kuwa sheria inawataka watendaji hao kusimamia haki hata pale inapotokea wanaotuhumiwa ni ndugu au rafiki zao.
“Shughulikieni mashauri ya walimu wanaotuhumiwa kwa kufuata haki. Kama haki inakutaka kupita katikati ya Mlima, pita hapohapo pasipo kupindisha, hata kama itakugharimu wewe mwenyewe,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Wakili Odongo amewasisitiza wajumbe hao kuhakikisha wanazingatia Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Na.25 ya mwaka 2015 pamoja na Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003 katika kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya walimu.
Sambamba na hilo, amesema Kamati husika zinapaswa kuzingatia Taratibu Bora za Uendeshaji wa Mashauri ya Nidhamu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2007 pamoja na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2009.
Awali, wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa TSC Prof. Willy Komba na Katibu wa Tume hiyo, Mwl. Paulina Nkwama, waliwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha kwamba wanaendelea kujenga taswira njema ya TSC kwa walimu kwa kutenda haki.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanalenga kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati husika ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia walimu kwa weledi.