Wakulima wakipima pamba mara baada ya kuvuna katika kata ya Kasekese
Wakulima wa pamba wakiwa katika mizigo yao wakisubiri kupima pamba katika kata ya Kasekese
…………………………………………………………………………..
Na Zilpa Joseph, Katavi
Jumla ya shilingi milioni arobaini na tano za malipo ya wakulima wa pamba kwa msimu wa mwaka 2020 zilizoibiwa na kiongozi mmoja wa Bodi ya Chama cha Msingi cha Wakulima (AMCOS) ya kata ya Kasekese wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi zitaanza kulipwa kesho baada ya fedha hizo kurejeshwa
Akizungumza na baadhi ya wakulima wanaodai fedha hizo Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Salehe Mhando amesema ili kuzuia tatizo kama hilo lisijitokeze tena kwa sasa viongozi wote wa bodi ya AMCOS watatoka katika kata hiyo
Mhando amesema malipo hayo yatafanyika kwa siku ya kesho Alhamis na Ijumaa na hivyo kuwataka wakulima hao wa pamba kuwajulisha wenzao ambao bado wanadai na ambao walipata malipo nusu
Ameongeza kuwa kwa kushirikiana na Bodi iliyopo sasa pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wamefanikiwa kurejesha fedha hizo ambazo tayari zimekwishalipwa katika akaunti ya AMCOS ya kata hiyo
Kwa upande wao baadhi ya wakulima wa zao la pamba ambao bado wanadai fedha zao wameeleza changamoto mbalimbali wanazopitia kutokana na kucheleshwa kwa malipo yao ikiwemo kuanguka kiuchumi na hivyo kushindwa kufanya shughuli nyingine za maendeleo kama walivyotarajia
Innocent Patrice ni mmoja wa wakulima wa pamba katika kata ya Kasekese amesema kuwa alilima pamba na kujaza gari aina ya Fuso matokeo yake aliambulia kulipwa shilingi milioni nne tu hali iliyosababisha familia yake kugoma kuendelea kulima pamba
Ameongeza kuwa kwa mwaka huu amelima shamba la ekari sita yeye peke yake kutokana na familia kukata tamaa
Naye Mchelle Kapaya mkulima wa kata hiyo ameiomba serikali kuongeza uangalizi hasa wakati wa kupima pamba ili wasiwe wanaibiwa katika mizani
“Utakuta mtu una pamba kilo mia sita halafu unaandikiwa kilo mia nne tunaomba hata hawa mabwana shamba wangekuwa wanakuja kuhakikisha pamba tuliyovuna tunapata kilo ngapi” alisema