******************************
Na Grace Semfuko,MAELEZO.
April 27, 2021.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul ameitaka Bodi ya Filamu Tanzania-TFB, kuibua vipaji vipya vya Wasanii wa filamu watakaoongeza nguvu katika tasnia hiyo ambayo amedai imekuwa na wasanii wachache.
Gelul amewataka Maafisa wa bodi hiyo kukutana na Maafisa Utamaduni wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa nchini, ambao wanaratibu wasanii hao ili kupata idadi halisi kwa kuwasajili na kuzitambua kazi zao.
Akizungumza katika ofisi za Bodi hiyo Jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Gekul amesema Tanzania inao wasanii wengi wa filamu ambao hawatambuliki, huku wanaofahamika wakiwa ni wachache tu tena ni wale wale wanaoonekana kila siku kwenye vyombo vya habari hivyo ipo haja ya kuwatambua na kuwaingiza kwenye kanzidata ya bodi ili waweze kupata haki sawa na wale wanaotambulika ambao idadi yao haizidi 300.
“Suala la usajili wa wasanii wetu ni la muhimu sana, nyinyi Bodi fikirieni kwenda mikoani kwenye Halmashauri zetu, msikae tu ofisini, fikeni kule ili muone vipaji mbalimbali vya wasanii wetu hawa wa uigizaji, wapo wengi na wana vipaji vizuri sana, lakini kuwafikia na kuwatambua inachukua muda mrefu, hii ni kwa sababu ya uelewa, Vijana wetu wengi huko bado hawafahamu kama kuna bodi inayowasaidia wasanii wetu, labda hawa wa Dar es Salaam pekee ndio wanajua” amesema Gekul.
Amesema kujua idadi ya wasanii wa filamu waliopo nchini ni hatua nzuri kwani wataingia katika kanzidata ambayo pamoja na mambo mengine kazi zao zitalindwa na wao watafaidika kulingana na matunda ya kazi zao huku pia Serikali ikifaidika kutokana na tozo mbalimbali za sanaa hizo.
“Ndugu zangu haipendezi kuwa mpaka leo hii hatujui idadi ya Wasanii wa Filamu katika nchi yetu, wakati ni kanzidata ambayo ukitafuta kwa Maafisa Utamaduni wa Wilaya wanakuletea, maana maafisa utamaduni hawa wanashinda nao huko, wakati wa matukio mbalimbali mfano Mwenge wanawaita na wanakuja japo huwa wanatengwa sana, lakini kuna watu wanapenda maigizo, sasa mkiwatumia hawa wanaweza kuwaletea idadi halisi ya kundi hilo” amesisitiza Gekul.
Aidha ameitaka bodi hiyo kutoridhishwa na idadi ndogo ya wasanii wa filamu iliyopo ambayo inaendelea kupungua kutokana sababu mbalimbali ikiwepo vifo na wengine kuacha kabisa fani hiyo hivyo waweze kuongeza kasi ya kusajili wasanii wengi zaidi watakaoleta jita katika fani hiyo.
“Tusiridhishwe na sura zile zile kila wakati, kwamba sinema inayochezwa kila siku ni ya mtu mmoja, ndiyo huyo huyo kila tv anaonekana yeye tu, kwa nini hao wengine wasionekane? ambao kimsingi tunatakiwa kuwajengea uwezo, kwa sababu hao tunaowategemea wanaweza kubadilisha mitazamo, wanaweza kusema wanabadili fani, kuna mtu anakwambia mimi kuanzia leo siimbi taarab naimba muziki wa dini, utamfanyaje? Sasa kama tunakosa kuwahamasisha wapya tutashindwa kufika mbali” amesema