……………………………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi, ametoa rai kwa wadau wote kushirikiana kwa pamoja kutafuta suluhu za changamoto za kiuchumi zinazovigusa vyombo vya habari.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo Aprili 28, 2021 Jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua semina ya wadau iliyoandaliwa kati ya Wizara na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi (UNESCO) kutengeneza vipaumbele vya Sekta hizo vitakavyoingia katika Mipango ya Kitaifa na Kimataifa hasa katika utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs).
“Mara chache sana tunapofanya semina na makongamano tunakumbuka kutathmini hili kwamba uhuru wa kiuchumi wa wanahabari ni muhimu sana, Mwanahabari ambaye analipwa kiduchu, hana uhakika wa mshahara, hana bima, hana pensheni kabla hajaenda kutafuta stori tayari hana uhuru” amesema Dkt.Abbasi.
Dkt. Abbasi ameongeza kuwa Semina hiyo italeta mapendekezo namna gani vyombo vya habari viimarishe mapato yao na uchumi wao uimarishwe na pia ni muhimu kuangalia dhana ya baadhi ya vyombo kuanzishwa kwa malengo ya mtu kisha akitimiza malengo hayo miaka miwili mitatu wanatasnia walioajiriwa wanaanza kutelekezwa na kubaki hoi.
“Leteni mawazo makini ili kile sisi Serikali tunachopaswa kufanya tukifanye na kinachopaswa kuanzia kwa wadau wa sekta wenyewe kianzishwe,” amesisitiza Dkt. Abbasi.
Katika semina hiyo ambayo ni maandalizi ya Siku ya Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yatakayofanyika Arusha Mei 3 mwaka huu, Dkt. Abbasi pia ametoa tuzo kwa wanahabari na wadau wa habari wanawake waliotoa mchango muhimu ambao ni Eda Sanga, Penzi Nyamngumi na Joyce Kiria.