**********************************
Na Silvia Mchuruza,
Bukoba.
Taasisi ya shule za Kaizirege na Kemebos yaahidi kuanzisha chuo cha elimu kitakachowasaidia vijana kusoma na kupata taaluma ya kazi.
Hayo yameelezwa na meneja wa shule ya Kaizirege na Kemebos Eulogius William Katiti katika mahafali ya tano ya kidato Cha sita, shule ya sekondari Kaizirege na Kemebos yaliyofanyika shuleni hapo.
Katiti amesema Mchakato wa kuanzisha chuo hicho upo katika hatua za awali na baada ya ukamilishwaji wa hatua hiyo ujenzi utaanza mara moja ambapo chuo hicho kitalenga wahitimu wa kidato Cha nne na cha sita, kitakachowasaidia vijana wengi kusoma na kupata taaluma ya kazi.
Aidha akipongeza hatua hiyo mgeni rasmi katika mahafali hayo shekhe wa mkoa wa Kagera Harouna Abdalla Kichwabuta amempongeza Mkurugenzi wa taasisi hiyo ya elimu Eusto Kaizirege Ntagalinda kwa mpango huo na kuwaomba wazazi kuwekeza katika elimu ili kuwa na wasomi wengi nchini.
“Ulimwengu huu ni wa wasomi wekezeni katika elimu, nawapongeza kufikiri mpango huo utakaoutambulisha mkoa wa Kagera” alisema Shekhe Kichwabuta.
Hata hivyo taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2007 ambapo jumla ya wahitimu 217 kutoka shule ya sekondari Kaizirege na Kemebos wamehitimu kidato cha sita katika shule hiyo.