Naibu waziri wa viwanda na biashara Exaud kigahe akiwaeleza jambo viongozi wa kiwanda cha Pareto kilichopo wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa alipofanya ziara ya kusaidia kutatua changamoto za kiwanda hicho
Na Fredy Mgunda,Mufindi.
Naibu waziri wa viwanda na biashara
Exaud kigahe amewahakikishia wamiliki wa kiwanda cha pareto kilichopo wilaya ya
Mufindi mkoani Iringa kuwa atawasaidia kutatua changamoto wanazokabiliwa nazo
katika uendesheji wa kiwanda hicho ambacho kimekuwa manufaa makubwa kwa
wananchi wa wilaya hiyo na taifa kwa ujumla.
Akizungumza mara baada ya
kumaliza ziara ya kutembelea kiwanda hicho naibu waziri Kigahe alisema kuwa amebaini kuwa kiwanda hicho
kinakabiliwa na changamoto mbalimbali kama kuwepo kwa biashara ya zao hilo
kimagendo na kusababisha wakulima kunyonywa na walanguzi hao.
Alisema kuwa walanguzi hao
wamekuwa wananua zao la pareto kwa bei ndogo huku wakitumia mizani ambayo
inawanyonya wakulima hivyo amepiga marufuku kwa walangiuzi hao kuacha mara moja
tabia hiyo ya kutumia mizani ambayo
haijathibitishwa na wakala wa vipimo.
Kigahe aliongeza kuwa serikali
itaweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wanawadhibiti walanguzi holela wa zao
la Pareto kwa kuwa wanashusha thamani ya zao hilo na kuwanyonya wakulima ambao
serikali imekuwa ikipambana kuhakikisha wanaongeza thamani ya wakulima.
Alisema kuwa kiwanda cha Pareto
kilichopo wilaya ya Mufindi kinauhitaji mkubwa wa zao hilo kwa kuwa hadi hivi
sasa wanapata Pareto kwa asilimia 50 tu tofauti na matarajio hivyo amewaomba
wakulima na wananchi wa wilaya hiyo na nyingine za mkoa wa Iringa kuchangamkia
fursa ya kulima zao hilo.
Kigahe alisema kuwa kilimo cha
zao la Pareto kinachukua muda wa miezi mitatu au minne kuvuna zao hilo ambao
linatumia gharama nafuu na kutoa faida kubwa kwa wakuma hivyo wakulima
wanahimizwa kulima kilimo cha Pareto.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Mufindi
Jamhuri Wiliamu alisema kuwa serikali ya wilaya itahakikisha kuwa walanguzi
holela hawaingii katika wilaya hiyo kwa lengo la kuhakikisha kuwa wakulima
wananufaika na nguvu zao wanatumia wakati wa kulima.
Alisema kuwa atakikisha
anaziagiza mamlaka husika kuthibiti wanunuzi wa zao la pareto wanaotumia mizani
ambayo haijathibitishwa na mamlaka ya udhibiti ubora.
Wiliam aliwaomba wananchi wa
wilaya hiyo kulima zao la Pareto kwa
wingi kwa kuwa linafaida kubwa katika kukuza uchumi wa mkulima na kuleta
maendeleo ya nchi.
Naye mhasibu wa kiwanda hicho
Gerald alimweleza naibu waziri na mkuu wa wilaya kuwa kiwanda hicho
kinakabiliwa wa ufinyu wa kupata mali ghafi za kiwanda hicho hivyo anaomba
serikali kutoa elimu kwa wananchi wa wilaya hiyo na mkoa wa Iringa kwa ujumla
kulima zao la Pareto kwa wingi.
Alisema kuwa hadi hivi sasa
kiwanda kinafanya kazi kwa asilimia 50 tu kutokana na kukosekana kwa malighafi
za kutosha kuendesha kiwanda hicho.
Alimalizia kwa kuomba naibu
waziri kuwadhibiti walanguzi holela ambao wamekuwa wakiwanyonya wakulima kwa
kutumia mizani ambayo haijakidhi vigezo vya mamlaka husika.