Baadhi ya wanawake wa kijiji cha Likwilo kata ya Kilosa wilayani Nyasa wakimuonesha ndoo tupu za maji Naibu waziri wa maji Mhandisi MaryPrisca Mahundi aliyevaa koti jeupe kama ishara ya uhaba wa huduma ya maji safi na salama katika kijiji hicho,wakati wa ziara yake ya siku mbili wilayani humo kukagua utekelezaji wa miradi ya maji,kushoto kwa naibu Waziri ni Mkuu wa wilaya ya Nyasa Esabela Chilumba.
Picha na Muhidin Amri
…………………………………………………………………………
Na Muhidin Amri,Nyasa
NAIBU Waziri wa maji Maryprisca Mahundi, amepokelewa na ndoo tupu za maji na wanawake wa kijiji cha Likwilo kata ya Kilosa wilayani Nyasa kutokana na kijiji hicho kutokuwa na huduma ya maji safi na salama kwa muda mrefu.
Naibu Waziri Mahundi, alikutana na hali hiyo jana wakati akiwa katika ziara yake ya siku mbili wilayani humo kukagua miradi ya maji inayotekelezwa na wizara ya maji kupitia wakala wa maji vijijini Ruwasa.
Kijiji cha Likwilo ni miongoni mwa vijiji katika 84 wilaya ya Nyasa, ambavyo tangu Uhuru mwaka 1961 havijawahi kupata maji ya bomba, badala yake wananchi wanalazimika kutumia maji ya visima vya asili na wengine kutumia maji ya ziwa Nyasa kwa matumizi ya kila siku.
Akiongea na wananchi hao,Naibu Waziri amewaomba kuwa wavumilivu wakati huu ambapo Serikali kupitia wizara ya maji imejipanga kuhakikisha inamaliza changamoto ya maji katika kijiji hicho na maeneo mengine ya wilaya ya Nyasa.
Alisema,wizara ya maji itatoa shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji katika mji mdogo wa Mbambabay makao makuu ya wilaya ya Nyasa ili kupunguza kero kubwa ya maji.
Amewaondoa wasiwasi wananchi hao juu ya fedha hizo na kusisitiza kuwa,zitaletwa ndani ya wiki moja kuanzia sasa ili kuanza utekelezaji wa miradi ya maji.
Aidha alisema,serikali itachimba visima viwili vya maji ili kukabiliana na changamoto ya huduma ya maji safi na salama,wakati ikusubiri mpango wake wa kutekeleza mradi mkubwa utakaotumia maji ya ziwa nyasa kusambaza maji katika maeneo mbalimbali katika wilaya ya Nyasa.
Katika hatua nyingine,Naibu Waziri amewashukuru wananchi wa kijiji hicho na kata ya Kilosa kwa kuonesha imani kubwa na Chama cha Mapinduzi kwa kuwachagua wagombea wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na kuwaomba kuendelea kuwa na imani na Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Kwa mujibu wake,wananchi wa jimbo la Nyasa hawakufanya makosa kumchagua Stella Manyanya kuwa Mbunge wa jimbo hilo, kwani ni mtu makini anayejua majukumu yake na kiongozi anayefanya kazi nzuri ya kuwatumikia wananchi.
Akizungumza kwa niba ya wananchi Mbunge wa jimbo la Nyasa Stella Manyanya alisema, jimbo la Nyasa ni kati ya maeneo yenye vyanzo vingi vya maji hapa nchini,lakini jambo la kusikitisha kuna kero kubwa ya maji safi na salama.
Hivyo,ameiomba wizara ya maji kuhakikisha ina maliza changamoto ya maji ili wananchi wapate nafasi ya kufanya shughuli zao za maendeleo badala ya kuendelea kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji jambo lililochangia sana kurudisha maendeleo yao.
Alisema, katika vijiji 84 alivyotembelea wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu mwaka jana, wananchi walimueleza kero kubwa ya maji maji safi na salama.
Ameiomba wizara ya maji kuwa na huruma na wananchi wa jimbo hilo ambao kwa muda mrefu wako katika mateso makubwa ya kukosa maji safi na salama kwani licha ya Serikali kwa nyakati tofauti kuanza kujenga miradi ya maji,bado changamoto ya maji kwa wananchi wa Nyasa ni kubwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Nyasa Fidelis Duwe alisema,kuna malalamiko makubwa ya wananchi kuhusina na ukosefu wa maji safi na salama kwani kati ya vijiji 84 vilivyofikiwa na maji ya bomba,vilivyofikiwa na huduma hiyo havizidi 10 na kila wanapokwenda kilio kikubwa cha wananchi ni kero ya maji.
Katika hatua nyingine,SERIKALI imetumia jumla ya shilingi milioni 390,870.000 kutekeleza mradi wa maji katika kijiji cha Chimate wilaya ya Nyasa ambao umeanza kuwanufaisha zaidi ya wakazi 2,798 wa kijiji hicho.
Meneja wa wakala wa usambazaji maji vijijini Ruwasa wilaya ya Nyasa Evaristo Ngole alisema hayo jana kwa naibu Waziri wa maji MaryPrisca Mahundi aliyetembelea mradi huo uliotekelezwa kwa fedha za malipo kwa matokeo(P4R) kwa kutumia mafundi wadogo.
Ngole alisema, maandalizi ya mradi wa maji Chimate ulianza mwezi Juni 2020 kwa kutayarisha vifaa vya ujenzi na kazi rasmi ya ujenzi ilianza Julai.
Ngole alitaja kazi zilizopangwa kutekelezwa katika mradi huo ni ujenzi wa chanzo cha maji,ujenzi wa tenki la mita za ujazo 75,kujenga vituo 15 vya kuchotea maji na ujenzi wa mtandao wa mabomba ya kusambaza maji urefu wa km15.50.
Alisema, hadi sasa mradi umekamilika kwa asilimia 85 na fedha zilizotumika ni shilingi milioni 356,112,310 kwa kujenga chanzo,kujenga tenki,vituo 18 vya kuchotea maji, na kujenga mtandao wa mabomba ya kusambaza maji na wanategemea kukamilisha ujenzi wa mradi huo ifikapo mwezi Mei.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa maji MaryPrisca Mahundi ameipongeza Ruwasa kwa kazi nzuri ya kutekeleza mradi huo na kuwataka wanufaika wa mradi kuwa walinzi wa miundombinu ili uweze kudumu kwa muda mrefu.
Alisema, wizara ya maji itaendelea kutekeleza miradi ya maji katika vijiji na maeneo mbalimbali kwa lengo la kumtua mama ndoo kichwani na kumaliza kero ya maji ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa baadhi ya wananchi kushindwa kufanya kazi za maendeleo.
Hata hivyo,akiongea kwa niaba ya wenzake mkazi wa kijiji hicho Andrew Mwarabu ameiomba Ruwasa kuongeza idadi ya vituo Vya kuchotea maji kutoka 18 vya sasa hadi kufikiwa 23 kutokana na idadi kubwa ya watu katika kijiji hicho.
Ameishukuru wizara ya maji kutekeeza mradi huo, kwani umemaliza kero ya maji iliyokuwepo na kuhaidi kutunza mradi kwa manufaa yao.