Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa kwanza kulia) akiwa
na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigella pamoja na viongozi
wengine wa mkoa huo, wakati Naibu Waziri Ulega alipotembelea eneo
unapowekwa mnada wa mifugo katika Kijiji cha Horohoro Kijijini kilichopo
kata ya Duga Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga na kuwataka wafanyabiashara
na wafugaji kutotorosha mifugo kwenda nje ya nchi kwa njia zisizo rasmi
kwani serikali inapoteza mapato.
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akifafanua juu
ya ujenzi wa mnada wa Kijiji cha Horohoro Kijijini katika Kata ya Duga
iliyopo Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga, kwa mkuu wa mkoa huo Mhe. Martine
Shigella na katibu tawala wa mkoa Bi. Judica Omari.
Muonekano
wa kibanda cha ushuru kilichosimikwa katika eneo la mnada wa Kijiji cha
Horohoro Kijijini uliopo Kata ya Duga Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga
ambapo shughuli mbalimbali zinaendelea ikiwemo ya kufyeka nyasi. Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ametembelea eneo hilo na
kusisitiza kuwa mnada huo utaanza kufanya kazi Mwezi Mei mwaka huu.
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Kulia), Mkuu wa Mkoa wa
Tanga Mhe. Martine Shigella (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe.
Thobias Mwilapwa wakibadilishana mawazo, mara baada ya Naibu Waziri
Ulega kufika katika ofisi za mkuu wa mkoa huo kabla ya kuanza ziara ya
kikazi ya siku moja Mkoani Tanga.
NA. MWANDISHI WETU, MKINGA
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amewataka wananchi wa Kijiji
cha Horohoro Kijijini Kata ya Duga katika Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga,
kutoruhusu mifugo ipitishwe kinyemela mpakani kwenda nchi jirani badala
yake wawafichue wanaofanya hivyo ili kuwadhibiti kwani serikali inakosa
mapato.
Ulega aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati
alipofanya ziara ya kikazi wilayani humo kwa kutembelea eneo lenye ekari
23 ambapo kutajengwa mnada wa mifugo kijijini hapo na kusema kuwa mnada
huo utakuwa chachu ya kuinua maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Alisema
lazima wananchi wilayani hapo kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri wa
kudhibiti mifugo kupitishwa kinyemela kwenda nje ya nchi ili kuiwezesha
serikali kukusanya mapato hatua ambayo itakuwa ni chachu kubwa kwao
kuwezesha maendeleo.
“Niwaambie tu kwamba lazima hivi sasa
tujipange kwa ujio wa fursa za mnada huu kwani baada ya miaka miwili
eneo hili litakuwa na picha tofauti na ilivyokuwa hapo awali na
litafungua ukurasa mpya wa maendelea kwenye eneo lenu na tumekubaliana
wizarani jambo hilo litaanza mwezi wa tano, wazee wa duga mtupe
ushirikiano kwa vijana wetu ambao watakuja kufanya kazi hapa.“ Alisema
Ulega
“RC Shigella utakuwa
umeacha alama kwa hili na nyinyi wananchi RC ametoa rai mnada huo
usigeuke kuwa ni dude ambalo litakuwa limekaa halina shughuli za kufanya
watu wanapitisha mifugo njia za panya na nyie mnawaona na hamtoi
taarifa kuzuia jambo hilo.” Alifafanua
Naibu Waziri huyo alisema
mnada huo ukianza kufanya kazi, eneo hilo litakuwa na shughuli
mbalimbali ambazo zitawasaidia kuwaingizia vipato mbalimbali vya
kimaendeleo hali ambayo itasaidia kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na
taifa kwa ujumla.
“Lakini niwaambie kwamba mkiacha watu
wanapitisha mifugo kwa njia ya panya hakuna nchi inachokipata na
wananchi hamuwezi kupata chochote hapo ni sehemu nzuri ya kuhakikisha
mnapaombea na kupiga dua, sala tuweze kuinua uchumi wetu watu wa
Mkinga.” Alisema
Aidha alisema mnada huo utaanza mwezi Mei
mwaka huu, huku akiwataka wakazi wa eneo la Kata ya Duga kuwapa
ushirikiano watumishi ambao watapelekwa kwa ajili ya kufanya kazi hiyo
ya kuhakikisha wanakusanya ushuru wa serikali.
Aliwataka pia
wafugaji wa eneo hilo kuhakikisha wanafuga kisasa ili waweze kuwa na
ng’ombe wenye tija zaidi kutokana na kwamba watanzania wapo kwenye
mazingira mazuri ya kufuga kisasa tofauti na nchi nyingine.
“Mhe.
Rais wetu Samia Suluhu Hassan anataka kuona ng’ombe wenye kilo 500
diwani wa Kata ya Duga na wengine tunataka tukimbie mchakamchaka tufikie
lengo la Rais anataka kuona tunauza nyama inatupa tija, mfugaji
anabadilika anapata kipato na nchi inapata mapato ya kutosha.” Alisema
Naibu
Waziri huyo alisema kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella
alibainisha kuwa mkoa unataka kufanya mambo mbalimbali ya maendeleo
lakini hayo yote hayawezi kufanikiwa ikiwa baadhi ya watu wanapitisha
ng’ombe kwenda nje ya nchi kinyemela kwa kutumia njia zisizo rasmi.
Alifafanua
kuwa ili kuongeza mapato ya serikali kupitia mifugo, katika mwaka ujao
wa fedha 2021/2022 Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepanga kutumia Shilingi
Bilioni 4 na Milioni 400 kwa ajili ya kujenga minada mbalimbali nchini
ukiwemo wa Kijiji cha Horohoro Kijijini kata ya Duga katika Wilaya ya
Mkinga Mkoani Tanga.
Alisema ujenzi huo unatokana na takwa la
kisheria la magonjwa ya wanyama namba 17 ya mwaka 2003 ambayo inataka
kufanyika hayo huku akieleza kuwa wizara ina mipango mingi ya
kuhakikisha wanawasaidia wafugaji kuhusu sehemu za malisho.
Awali
akizungumza katika eneo hilo la mnada Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine
Shigella alisema moja ya tatizo kubwa lililopo eneo la mpakani ni
kutokuwa na mnada wa uhakika kwa ajili ya wafanyabiashara na wafugaji wa
mifugo, ndiyo maana serikali ya Mkoa wa Tanga na Wizara ya Mifugo na
Uvuvi zinataka kusiwe na ufugaji wa kuhamahama.
Shigella
alisema hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan aliyoitoa bungeni hivi karibuni, ameeleza nia yake ya
kutaka kuona wafugaji matajiri na siyo wa kuhamahama na ili kuweza
kujenga mazingira wezeshi ya eneo la kuuzia mifugo kwani bila kufanya
hivyo, wafanyabiashara wamekuwa wakienda kuwalangua wafugaji kwenye
mazizi yao na hivyo kujikuta hawanufaiki ipasavyo.
“Kuna
soko kubwa nchini Kenya ambapo baadhi ya wafugaji na wafanyabiashara
wasiokuwa waaminifu walikuwa wanasafirisha mifugo kwenda Kenya na baadhi
ya watumishi wa serikali wasiokuwa waaminifu ndio walikuwa wanaongoza
mchakato huo wa kusafirisha mifugo bila kupitia kwenye taratibu mahususi
zilizopo.” Alisema Shigella
Hata hivyo alisema anaishukuru
wizara kwa kuliona hilo na kuunda kamati na kuweza kubaini uwepo wa
changamoto walizokuwa wanalalamikia wafanyabiashara na wananchi wa
Kijiji cha Horohoro Kijijini kwani kubwa walilokuwa nalo ni mifugo
kupitishwa kwenye njia isiyokuwa rasmi, kutokana na kutokuwa na eneo
maalumu ambalo mifugo kabla haijasafirishwa inatakiwa ipumzishwe mahali
ambapo itakaguliwa magonjwa na kukusanywa kwa tozo kabla ya kusafirishwa
kwenda nchi jirani.
Kwa upande wake Afisa Biashara wa Minada
kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Basil Mataba alisema wizara ina
jumla ya minada ya upili 14 na minada 11 ya mpakani ambapo mnada wa
Kijiji cha Horohoro Kijijini mara utakapoanza kufanya kazi utakuwa wa
12.
Bw. Mataba alisema wanategemea Mwezi Mei mwaka huu mnada
wa Kijiji cha Horohoro Kijijini utaanza kufanya kazi hivyo kuondoa adha
ambazo walikuwa wakizipata wafanyabiashara na wafugaji kutorosha mifugo
kwenda nje ya nchi ili kuuza mifugo yao.
Alibainisha hadi sasa
eneo hilo la mnada tayari shughuli mbalimbali zinaendelea ikiwemo ya
kufyeka nyasi na tayari kibanda cha kukusanyia ushuru kimeshasimikwa
wakati wakiendelea na ujenzi wa eneo hilo huku akieleza kwamba wizara
itaendelea na hatua za ununuzi wa vifaa kwa ajili ya uzio wa awali.