Home Mchanganyiko MILIONI MIA TATU KUPUNGUZA KERO YA MAJI LIKWILU

MILIONI MIA TATU KUPUNGUZA KERO YA MAJI LIKWILU

0

***************************

Serikali imeahidi kupeleka shilingi milioni mia tatu katika kijiji cha Likwilu kilichopo Kata ya Kilosa, Wilayani Nyasa mkoani Ruvuma ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Likwilu Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Maryprisca Mahundi (Mb) amesema kutokana na shida ya maji inayowakabili wananchi wa Likwilu hususan kina mama, serikali italeta milioni mia tatu za kuanzia.

“Wiki ijayo Katibu Mkuu Wizara ya Maji ataleta shilingi milioni mia tatu kwa ajili ya kujenga tanki litakalo kuwa na ukubwa mzuri wa kupokea maji kutoka Ziwa Nyasa, kujenga vituo vya kuchotea maji na fedha itakayobaki tutawasogezea huduma wananchi wengine ambao wanashida ya maji kama hapa Likwilu na kuchimba kisima kimoja cha haraka kwa ajili ya kijiji cha jirani, Waziri Mahundi amesema.

Amesema mradi huu utafanyika ili kupata suluhisho la muda mfupi ili kuleta matokeo ya haraka na kuwawezesha wananchi kupata majisafi na salama wakati utaratibu wa kupata mradi mkubwa zikiendelea.

Pamoja na hayo, Waziri Mahundi amemuagiza Meneja wa RUWASA mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshanga kuhakikisha fedha zitakapofika zinatumika kujenga tanki, kusambaza mtandao wa maji, na kuchimba kisima ili wananchi wa Likwilu wapate majisafi na salama na yenye kutosheleza.

Hali ya upatikanaji ya huduma ya majisafi na salama Wilayani Nyasa hadi kufikia mwezi Machi, 2021 ni asilimia 52.

Waziri Mahundi yupo Wilayani Nyasa mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi kukagua miradi ya maji na kuangalia changamoto kubwa ya ukosefu wa majisafi na salama kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa.