…………………………………………………………………………………………
Na. Angla Msimbira – ARUSHA
Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia ,Wazee na watoto Mhe. Dorothy Gwajima amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha inatenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa dawa ya kuua mazalia ya viluilui wa mbu waenezao Malaria ili kupunguza na kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa malaria nchini.
Ametoa agizo hilo wakati akihutubia wananchi ikiwa ni siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani yaliyofanyika kitaifa Jijini Arusha, yenye kauli mbiu ya “Ziro Malaria inaanza na mimi, Nachukua hatua kuitokomeza”.
Katika maadhimisho hayo Dkt. Gwajima amesema kuwa dawa hizi zinatakiwa kufika kwa viongozi wa vijiji na kata ili kuhamasisha jamii umuhimu wa utuzaji wa mazingira kwa kuuwa mazalia ya mbu nchini.
Amefafanua kuwa wananchi wakihamasishwa juu ya matumizi sahihi ya dawa ya kuulia vimelea vya mbu nchini kutasaidia kupunguza ugonjwa wa malaria kuanzia ngazi ya familia na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wa mafanikio yaliyofikiwa yaliyofikiwa na Wizara yake Dkt. Gwajima amesema wamegawa vyandarua Katika halmashauri 50 na kuweza kuwafikia wananchi milioni 15.3 na hivyo kuwakinga watu takribani milioni 15.6 kupitia kampeni maalumu,pia wamegawa vyandarua milioni 3.7 kupitia vituo vya kutolea huduma za afya vya Umma kwa wajawazito na Watoto chini ya mwaka mmoja wanaohudhuria kliniki.
Kwa upande wa upuliziaji wa dawa za ukoko Kwenye ukuta ndani ya nyumba amesema jumla ya nyumba 552,643 zimepuliziwa na hivyo kutoa Kinga kwa watu milioni 2.5.
Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshugulikia afya Dkt Grace Magembe ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatenga bajeti kwa ajili ya afua za kujikinga na maambukizi ya malaria nchini.
Amesema kuwa Halmashauri ambazo hazitatenga fedha kwa ajili ya afua mbalambali za afua hizo Serikali haitasita kuzirejesha bajeti hizo mpaka pale watakapotenga fedha hizo.
Dkt Magembe amesema kuwa nguvu kubwa inahitajika kuwekwa katika kata ambazo bado tatizo kubwa la maumbukizi ya ugonjwa huo , hivyo vi nyema halmashauri zikahakikisha zinatenga fedha za kutosha kwa lengo la kupunguza maambukizi ya malaria nchini.
Aidha. Dkt, Magembe amesema kuwa Halmashauri zimeendelea kutekeleza Sheria ya afya ya Jamii ya mwaka 2009 hususani kipengele kinachohusu usimamizi , udhibiti na usafi wa mazingira ili kuzuia mbu na wadudu wanobeba vimelea vya magonjwa kuzaliana.
Dkt Magembe amesema kuwa bado kuna halmashauri chache ambazo bado ugonjwa wa malaria ni tatizo, hivyo Serikali itahakikisha inaweka nguvu katika kuhakikisha wanasimamia ili kupunguza maambukizi ya malaria.
Ameendelea kusema kuwa Halmashauri zetu zimekuwamstari wa mbele katika kutunga sheria na kuzisimamia usafi wa mazingira, kaya, kata, masoko , ofisi za umma katika maeneo ya bishara haya yote yamelenga katika kuhakikisha wanatokomeza maambukizi ya Malaria.
Kwa upande mwingine, amewataka wananchi kuhakikisha wanatumia vituo vya afya kwa ajili ya kupima afya zao, kwa kuwa serikali imewekeza fedha nyingi katika kuhakikisha wanajenga miundombinu.