BARAZA Kuu la Waislamu (BAKWATA), Mkoa wa Mwanza, limetoa msaada wa futari na daku (vyakula anuwai)na vitu mbalimbali kwa ajili ya wafungwa na mahabusu katika Gereza Kuu la Butimba.
Msaada huo wa vyakula,(mchele,unga wa ngano, sukari na mafuta ya kula),sabuni, vitabu vya Kuran Tukufu, kabati, nguo, sabuni na maturubai kwa ajili kuswalia ulikabidhiwa kwa Mkuu wa Gereza hilo, Sunday Mwakasegule, juzi.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikh Hasani Kabeke,alisema unawalenga mahabusu na wafungwa waliofunga saumu ya Mwezi Ramadhani ingawa wamekuwa wakipeleka misaada gerezani hapo si kwa imani ya dini, la hasha.
Pia msaada huo ni unaunga mkono serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan,kutokana na uhusiano mzuri na taasisi mbalimbali za dini eneo ambalo inafanya vizuri.
“BAKWATA ni chombo kinachosimamia taasisi zote za Kiislamu na Waislamu, tumekuwa na utamaduni na utaraibu wa kujikusanya Mwezi wa Ramadhani kwa kuwajali ndugu zetu waliopo gerezani wengine wakiwa wamekuhumiwa na baadhi wakisubiri kuhukumiwa kwa makosa waliyotenda,”alisema Sheikh Kabeke.
Alisema kuwa Waislamu wa Mkoa wa Mwanza wameguswa na kuona washiriki jambo hilo kwa futari na daku kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kuwajali ndugu zao waliopo gerezani kwa makosa mbalimbali ambao wamediriki kufunga saumu.
Aidha aliwataka wafungwa na mahabusu (waislamu na wasio waislamu) wawe na subira kwani yaliyowakuta pia yamewakuta watu wema na wazichukulie adhabu zao kama shule ya mafunzo ili wakirejea kwenye jamii wawe watu wema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza Kuu la Butimba, Sunday Mwakasegule,aliishukuru BAKWATA kwa msaada huo mkubwa uliotokana na vipato vyao, kwamba wanauthamini na kuahidi utawafikia walengwa wote.
“Msaada huu umetokana na vipato vyenu ambavyo mara nyingi matumizi huwa makubwa sababu ya mahitaji ya kibinadamu na familia zenu,lakini mmeamua kuziweka pembeni familia na kuja kuwaona ndugu zenu wanaotaabika gerezani kipindi hii cha neema,”alisema Mwakasegule.
Alisema ingawa yeye ni Mkristo anayeamini Mungu ni mmoja,Mwezi wa Ramadhani ni wa neema na amekuwa akitafakari hivi kweli chini ya jua,neema hiyo inamkwepa na inawalenga Waislamu pekee bali na yeye yumo kwa sababu ya kutenda mema.
Mkuu huyo wa gereza alisema kitendo cha waumini wa kiislamu kuwakumbuka ndugu zao,wawaone ni jamii ya Watanzania,wamo gerezani kwa makosa na pengine hata sisi tunayatenda ya unyanyasaji wa wanawake kwa vipigo ama kuwapa mimba wanafunzi, isipokuwa arobaini hazijafika.