………………………………………………………………………..
Nuru Mwasampeta na Steven Nyamiti – Dodoma
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampuni kubwa na ndogo zinazowekeza kwenye sekta ya madini.
Waziri Biteko ametoa wito huo leo tarehe 23 Aprili, 2021 alipokutana na uongozi wa juu wa Benki ya NMB uliofika kwa nia ya kutaka kujua maeneo ya ushirikiano baina ya wizara na benki hiyo ili waweze kushiriki katika kuinua uchumi wa nchi kupitia sekta ya madini kwa kutoa mikopo kwa wawekezaji hao.
“Niwasihi sana ndugu zangu, unganeni mfanye kazi kwa pamoja Benki hii itatoa asilimia 20 nyingine 30, 40, 10 kwa mwekezaji na hivyo manufaa ya uwekezaji kupitia sekta ya madini yataonekana zikikopwa nje ya nchi manufaa wanapata mataifa mengine” alisisitiza.
Amesema wizara imekuwa ikipokea wawekezaji wengi wenye changamoto za mitaji na wakielekezwa kukopa kwenye benki za ndani kutokana na sera yetu ya local content wanakiri benki za ndani hazina uwezo wa kukopesha kiasi cha pesa wanachokihitaji.
Akizungumza katika kikao hicho Waziri Biteko ameweka wazi kuwa biashara ya uchimbaji wa madini inahitaji mtaji mkubwa na kubainisha sifa kuu tatu za biashara hiyo kuwa ni biashara inayohitaji mtaji mkubwa (capital intensive), muda wa kutosha mpaka kuona matokeo pamoja na uwepo wa rasilimali watu ya kutosha.
Biteko ameushukuru uongozi wa Benki ya NMB kwa kuona umuhimu wa kufika na kuzungumzia masuala ya muhimu kama ya mitaji na kuona kuwa Sekta ya Madini ni mahala wanapoweza kuwekeza fedha zao.
Aidha, amesema Wizara pamoja na taasisi zake wako tayari kufanya kazi bega kwa bega na benki za ndani na kuwaongoza mahala penye viashiria vizuri ili waweze kuwekeza pesa zao na kukiri kuwa wizara yake haitakuwa tayari kuziingiza benki katika kutoa mikopo mahala ambapo kuna viashiria hatarishi vya hali ya juu maana haipendi benki hizo kupata hasara. “Kazi ya wizara ni kuzishauri benki nasisi tutafanya hivyo” alisisitiza.
Akibainisha maeneo ambayo yana viashiria vizuri katika biashara ya madini Biteko amesema ni pamoja na eneo la uchakataji wa madini, uongezaji thamani wa madini biashara ya madini na kubainisha kuwa katika hatua hizo tayari mwekezaji anakuwa na uhakika wa kile anachokifanya hivyo ni rahisi kuuza madini aliyonayo na kupata pesa ya kulipia deni la mkopo aliouchukua.
Ameitaka Sekta ya Benki kushirikiana na wizara katika kusukuma gurudumu la maendeleo na kusema kazi haiwezi kwenda mbele wala kujulikana kusipokuwa na ushirikiano baina ya sekta hizo mbili. Tushirikiane kwa pamoja, tusukume gurudumu, sekta iende mbele ili sote tuone manufaa, alisema.
Akibainisha vipaumbele vya wizara, Biteko amesema kuwa kwanza ni kutengeneza ajira kwa watanzania. Amebainisha kuwa endapo kuna leseni imetolewa kwa mwekezaji na haifanyiwi kazi leseni hiyo inanyang’anywa na kupewa wachimbaji wadogo walio tayari kufanya kazi.
Pili amesema kipaumbele kingine ni kubadilisha mtazamo wa wachimbaji wadogo katika suala zima la nidhamu ya pesa. Katika hilo ameitaka benki hiyo kuendesha mafunzo mbalimbali kwa wachimbaji wadogo katika eneo hilo ili kuwawezesha na kuwasaidia kuweza kufanya kazi kwa weledi na baadaye walipe kodi zitakazochangia katika maendeleo ya nchi.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila ameutaka uongozi wa benki hiyo kuwasilisha chati inayoonesha viwango vya chini na vya juu vya mikopo inayoweza kutolewa na benki hiyo kwa wawekezaji ili pindi wawekezaji wenye nia ya kukopa wanapotembelea ofisi yake wanakuta taarifa hizo muhimu na kufanya mawasiliano.
Aidha, ameishauri benki ya NMB kujihusisha na biashara ya bima na kukiri kwamba biashara hiyo ni fursa ya wazi na itawawezesha kutengeneza pesa na kuendeleza benki yao kiurahisi.
Akiwasilisha hoja zake kwa uongozi wa wizara, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna ameanza kwa kutoa pongezi kwa Sekta ya Madini na kusema kwamba sekta ya madini imeibeba nchi hususani katika kipindi cha janga la corona katika suala zima la kuiingizia nchi pesa za kigeni. Amesema sekta hii imekuwa ni tegemeo sana katika suala zima la pesa za kigeni. “Sisi tupo kwenye sekta ya fedha hivyo tunaona namna sekta hii ilivyokuwa mkombozi” amesisitiza.
Amesema awali benki ya NMB ilikuwa ikisita kuingiza mkono wake kwenye sekta ya madini lakini kutokana na namna bora zilivyowekwa katika suala zima la mnyororo wa biashara ya madini benki hiyo imeamua kuingia na kutoa mikopo ili kuwawezesha wafanyabiashara na wachimbaji wa madini kufanya biashara kwa ufanisi ambapo mpaka sasa tayari benki hiyo imetoa mikopo ya shilingi bilioni 10 kwa wachimbaji wadogo.
Aidha, amesema benki hiyo ikishirikiana na benki kutoka Afrika ya Kusini wametoa mkopo wa dola za kimarekani milioni 22 kwa mgodi wa Uchimbaji Mkubwa wa madini wa Geita (GGM).
Zaipuna amebainisha kuwa, kwa sasa benki yao ina mtaji wa shilingi trilioni 1.1 ambapo ameonesha imani yake ya kuchangia katika miradi mikubwa ya uchimbaji na kuboresha maisha ya watanzania.
Amesema benki yake inaweza kutoa mkopo wa kiasi cha shilingi bilioni 240 bila shida yoyote.
Amekiri kuwa biashara ya madini ina changamoto kubwa katika kuielewa, kutokana na changamoto hiyo benki hiyo imefanya jitihada ya kuwasaidia watumishi wake kuielewa biashara ya madini kwa kuandaa mafunzo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwepo wizara na taasisi zake ili kuwajengea uwezo na uelewa wa namna biashara ya madini inavyofanyika.
Akihitimisha mazungumzo yake Ruth Zaipuna amesema ofisi yake ipo tayari kuisikiliza wizara kadri itakavyoona inafaa kuona ni maeneo yapi yapewe kipaumbele ili waweze kushirki katika kulisukuma gurudumu la maendeleo kupitia benki anayoisimamia.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Yahya Samamba amekiri kufanya mafunzo kwa wataalamu wa benki hiyo na kuwaelimisha juu ya mnyororo mzima wa biashara ya madini unavyofanyika.