…………………………………………………………………………..
Na Richard Mwamakafu – WHUSM, Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ametoa pongezi kwa Tume ya Ushindani nchini (FCC) na Timu ya Soka ya Simba SC kwa kumaliza mgogoro wao na kusisitiza vilabu vingine vya soka kuiga mfano huo ili kuleta maendeleo ya mchezo wa soka nchini.
Mhe.Bashungwa ametoa pongezi hizo leo Aprili 24, 2021 alipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha michezo cha Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) kilichopo Kigamboni, Dar es Salaam
“Navikaribisha Vilabu vingine kushirikiana na Serikali ili kuendana na Dira ya Serikali na maelekezo ya Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kutaka Sekta hii kutoa ajira kubwa sana kwa vijana na kuchangia kwenye pato la nchi”
Mhe.Bashungwa ametumia nafasi hiyo pia kuipongeza timu ya Simba kwa kufika hatua ya robo fainali katika Michuano ya Klabu Bingwa Afrika, huku akiwasihi Watanzania kuonyesha uzalendo wa kuiunga mkono timu hiyo inayoitangaza nchi ya Tanzania kimataifa na kupitia kauli mbiu ya timu hiyo ya (Visit Tanzania) “Tembelea Tanzania” katika Jezi zao.