Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwegamile Kata ya Bwigiri Wilaya ya Chamwino alipofika katika kijiji hicho kutoa maamuzi ya mgogoro wa ardhi kati ya wananchi, halmashauri na muwekezaji wa kiwanda cha Mega Bevareges LTD.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge wa pili akiongozana na wajumbe na viongozi mbali mbali wa Mkoa na Wilaya ya Chamwino kukagua mipaka na kupokea ripoti ya kamati iliyoundwa kuchunguza mgogoro huo kati ya wananchi, halmashauri na muwekezaji.
Baadhi ya viongozi wakipitia nyaraka mbalimbali zinazoonyesha mipaka ya ardhi wakati akitatua mgogoro wa ardhi uliokuwepo kati ya wananchi, halmashauri na muwekezaji wa kiwanda cha Mega Bevareges LTD.
Mwenyekiti wa kamati maalumu iliyoundwa kufuatilia mgogoro wa kati ya wananchi, halmashauri na muwekezaji wa kiwanda cha Mega Bevareges LTD. Bw. Aron Kameta akizungumza wakati akiwasilisha ripoti ya uchunguzi wakati ya mkutano huo.
Mjumbe wa kamati maalumu iliyoundwa kufuatilia mgogoro kati ya wananchi, halmashauri na muwekezaji wa kiwanda cha Mega Bevareges LTD. Kutoka kundi la wananchi Bw. Gabriel Masinga akizungumza wakati wa mkutano kati ya wananchi na Mkuu wa Mkoa kijijini hapo.
……………………………………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Chamwino
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge ameamuru wananchi wa Kijiji cha Mwegamile Kata ya Bwigiri Wilaya ya Chamwino kupewa ardhi yenye ukubwa wa ekari 605 ambayo awali ilikuwa ikimilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ili waitumie kuendeshea shughuli za kilimo.
Dkt Mahenge ametoa agizo hilo Wilayani Chamwino mara baada ya kupokea taarifa na mapendekezo kutoka kwa kamati maalumu aliyoiunda mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu kufuatilia mgogoro wa ardhi ulioibuka kati ya wanakijiji cha Mwegamile, halmashauri ya Chamwino na muwekezaji wa kampuni ya Mega Beverages Limited inayozalisha vinywaji vikali inayotaka kuwekeza katika eneo hilo kiwanda Cha mvinyo na mashamba ya zabibu.
Taarifa ya Kamati inaonesha eneo hilo la ekari 605 ambalo ni sehemu ya shamba kubwa lenye jumla ya ekari 1622 lilikuwa likimilikiwa na halmashauri ya Wilaya ya Chamwino tangu mwaka 1984 na kupewa kampuni kadhaa za uwekezaji ambazo zilishindwa kuwekeza ndipo likarudishwa katika umiliki wa halmashauri ambayo pia ilishindwa kuliendeleza na hivyo wananchi wakaingia na kuanza kulitumia kulima na kuanza kujimilikisha.
“Kwahiyo kamati imejiridhisha pasina shaka eneo hilo ni mali halali ya Halmashauri lakini baada ya kushindwa kuliendeleza wananchi wakaanza kulimiliki kwa mda mrefu, hapa walikaa mababu na wajukuu wakazaliwa hapa ndio maana wanahisi ardhi ni mali yao” amesema Dkt Mahenge.
Amesema mgogoro uliibuka rasmi mara baada ya halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kupata Muwekezaji wa kutengeneza vinywaji wa Kampuni ya Mega Beverages limited na Halmashauri kumuuzia ekari 4000 kutoka kwenye eneo hilo ndipo wananchi wakapinga na kudai ardhi hiyo ni mali yao wakitaka ufafanuzi wa muwekezaji kupewa eneo hilo.
Amesema kamati imepitia katika eneo lote lenye ukubwa wa ekari 1622 na kuja na mapendekezo ya muwekezaji huyo kupewa eneo lake alilolinunua la ekari 400, kwa ajili ya uwekezaji katika kilimo cha zao la zabibu na ujenzi wa kiwanda, na wananchi kuachiwa ekari 605 ili waendeshe kilimo Cha zabibu na halmashauri kubakiwa na ekari 617 kati ya ekari 1622 zilizopo katika eneo hilo.
Mara baada ya maridhiano hayo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge ameruhusu muwekezaji huyo kuendelea na shughuli za ujenzi wa miondombinu na maandalizi ya mashamba mara baada ya awali kusitisha shughuli hizo ili kupata maridhiano katika pande zote tatu baada ya kuibuka mgogoro huo.
Aidha ametoa wiki mbili kwa kamati hiyo kufanya tathmini ya eneo la ekari 605 litakalogaiwa kwa wananchi ili kubaini kama kuna watu walikuwa wakilimiliki, sambamba na kufanya tathmini ya watu walioathirika katika eneo alilopewa muwekezaji ili wapewe ARDHI kwenye eneo la ekari 605 zilizotolewa kwa wananchi.
“kamati musimamie zoezi hili kikamilifu kuhakikisha wale walioathirika na eneo alilopewa mwekezaji ndio wapewe kipaumbele katika kupewa eneo lenye ekari 605, pia mpitie kuona kama eneo hilo hakuna wananchi wanaomiliki eneo hilo tusije kutengeneza mgogoro mwingine” alisema Dkt. Mahenge.
Sambamba na hilo Dkt Mahenge amemtaka muwekezaji kuanza shughuli zake huku akitimiza makubaliano yake na halmashauri ya muda wa uwekezaji kwa kufuata masharti yote ikiwamo muda aliopewa kukamilisha ujenzi na kuanza kazi.
“Sisi tunataka wawekezaji hivyo ukafuate taratibu zote ulizopewa na halmashauri za kiuwekezaji, pia maelekezo yangu unapoendelea na ujenzi kuna mazao ya wakulima mazao yasiguswe mpaka yatakapo vunwa” amesema.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa muwekezaji kwani kiwanda hicho kina umuhimu mkubwa kwa jamii kwa kupata ajira na pia wataweza kuuza mazao yao katika kiwanda hicho na kupata kipato hasa baada ya ongezeko la viwanda vya kuchakata zabibu Mkoani Dodoma kuongezeka itaongeza ushindani.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya kufuatilia mgogoro huo Bw. Aroni Kameta amesema walipewa adidu 9 za kutekeleza katika kutatua mgogoro huo na waliweza kuwahoji watu katika ngazi tofauti tofauti pamoja na muwekezaji huyo na kupata taarifa mbalimbali zilizowezesha kuja na ushauri uliotolewa.
Aidha kamati imeshauri halmashauri kuwajengea uwezo viongozi ngazi za vijiji katika utunzaji wa nyaraka zinazohusu ardhi na mambo mengine kwa kumbumbu ya baadaye kwani kuna baadhi ya nyaraka zilihitajika hazikupatikana kutokana na kupotea, pia hiyo itawasaidia kuwepo kwa taarifa baada ya kubadilishana uongozi.
Nae mjumbe katika kamati hiyo kutoka kundi la wananchi bw. Gabriel Masinga amesema kutokana na nchi yetu kusifika kwa kuwa na amani na maridhiano wameshirikiana na kamati hiyo na kuja na maamuzi yenye manufaa kwa pande zote tatu yani wananchi, muwekezaji na halmashauri.