Mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU Bregedia Jenerali John Mbungo akikabidhi baadhi ya fedha zilizookolewa kwa tasisi husika.
Mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo akizungumza wakati wakukabidhi fedha hizo
Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Arusha James Ruge akiongea katika tukio hilo la kukabidhi fedha.
…………………………………………………………………………………………
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya kupambana na Kuzuia Rushwa mb nchini(TAKUKURU) Bregedia Jenerali John Mbungo amekabidhi shilingi bilioni 1.36 kwa taasisi sita ikiwemo PSSF, NSSF, TRA, Vyama vya ushirika pamoja na dhuluma dhidi ya wananchi.
Akikabidhi fedha hizo Bregedia Jeneali Mbungo alisema kuwa fedha hizo ni fedha za umma na kodi mbalimbali za serikali zilizokuwa zimechepushwa kwa njia ya rushwa na kufanyiwa ubadhilifu na watuhumiwa mbalimbali kinyume na sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Aidha alikabidhi shilingi milioni 212 kwa mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma(PSSF) ambapo alieleza kuwa fedha hizo ni kati ya shilingi milioni 293 ambazo wameziokoa katika uchunguzi wao kufuatia vitendo vya vya Rushwa vilivyopelekea uingiaji wa mikataba mibovu pamoja na udanganyifu wa dhamana.
“Fedha hizi zilichepushwa kwa njia ya Rushwa na waajiri wasio waaminifu na kujinufaisha wao binafsi kinyume na sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na pia fedha hizi ni sehemu ya shilingi bilioni 1.86 zilizotolewa kinyume na taratibu zinazosimamia vyama vya ushirika zikiwemo saccos za AUWSA na AICC,”Alisema Generali Mbungo.
Alisema kuwa pia wamefanikisha ulipaji wa zaidi ya milioni 7.6 ambazo ni fedha za mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii(NSSF) fedha ambazo ni makato ya michango ya watumoshi yaliyopaswa kuwasilishwa katika mfuko huo tawi la Arusha kama ambavyo sheria zinaelekeza lakini zilichepushwa na waajiri kwa njia ya Rushwa.
“Nitoe rai kwa waajiri wote nchini kuhakikisha kuwa wanawasilisha michango ya akiba za waajiri wao katika mifuko stahiki ya hifadhi ya jamii kwani kutenda kinyume ni kosa la Rushwa kwa mujibu wakifungu cha 31 cha sheria ya TAKUKURU na 11 ya mwaka 2007,” Alieleza.
Katika hatua nyingine Generali Mbungo alikabidhi milioni 11 ambazo ni sehemu ya shilingi 112 ambazo ni fedha za umma za Trekta zilizotolewa na mfuko wa pembejeo wa taifa zilizostahili kurejeshwa serikalini.
Pia katika uchunguzi walioufanya jijini hapa kwa kushirikiana na mamlaka ya mapato Tanzania(TRA) wamebaini makosa ya Rushwa ya ubadhilifu pamoja na uhujumu uchumu yaliyosababisha upotevu wa fedha ya kodi ya serikali zaidi ya shilingi milioni 519 ambao wahusika ni makampuni ya utalii, ujenzi na kilimo yaliyopo mkoani hapa.
Sambamba na hayo pia alikabidhi fedha shilingi milioni 227.8 za wananchi ambazo zilitokana na dhuluma, fedha za vyama vya ushirika SACCOS na AMCOS milioni 50.1ambapo alitoa rai kwa viongozi wa vyama hivyo kuhakikisha wanaweka utaratibu ulio wazi katika ukopeshaji na urejeshaji wa fedha za vyama vyao.
Aliendelea kusema kuwa TAKUKURU mkoa wa Arusha inaendelea na uchunguzi unahusu tozo za vibali vya ujenzi, utoaji wa ushuru wa huduma pamoja na ushuri wa uzoaji taka ambapo katila eneo hilo wameshafanikiwa kuokoa fedha za halmashauri ya wilaya ya Arumeru milioni 117.8 ambazo zilikuwa hatarini kuhujumiwa kwa njia ya Rushwa na baadhi ya watumishi na wazabuni.
Wakati huohuo alikabidhi nyaraka za umiliki wa viwanja vitatu vyenye thamani ya shilingi milioni 18.5 mali ya Alex Robert, Emmanuel Segeja na Bertha Pallangyo wote wakiwa ni wakazi wa wilaya ya Arumeru ambapo pia alikabidhi kadi za ATM 100 za benki ya NMB na CRDB zilizochukuliwa na wanufaikaji kinyume na matakwa ya taratibu za kibenki.
Hata hivyo tasisi zilizorejeshewa fedha pamoja na wananchi wameishukuru TAKUKURU kwa jitihada za kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa na kukabidhiwa kama ilivyotakiwa kufanyika awali.