………………………………………………………………………………..
Timu ya Mbeya Kwanza imekuwa ya kwanza kupanda Ligi Kuu Tanzania bara Msimu ujao baada ya kuichapa bao 1-0 African Sports katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Mabatin, Pwani.
Shujaa wa Mbeya Kwanza aliyeipeleka Ligi Kuu ni Willy Edger dakika ya 75 na kuwafanya mashabiki na wanachama wa timu hiyo kulipuka kwa shangwe.
Kwa ushindi huo Mbeya Kwanza imefikisha Pointi 38 na kuwaacha African Sports wakiwa nafasi ya pili na Pointi zao 28 ambazo zinawapa nafasi nzuri ya kuwania hatua ya mtoano katika michezo mitatu iliyosalia.
Mbeya Kwanza ilianzishwa mwaka 2012 ikiitwa Coca Cola Kwanza kama timu ya wafanyakazi wa Coca Cola, lakini mwaka 2014 ilibadilishwa na kuitwa Mbeya Warriors ikiwa inashiriki Ligi ya Mabingwa wa Mkoa (RCL).
Hata hivyo mwaka 2015 ikiwa Ligi Daraja la Pili (SDL) ikabadilishwa na kuwa Mbeya Kwanza ambapo jina hilo limeendelea hadi sàsa.
Msimu uliopita Mbeya Kwanza ilimaliza nafasi ya nne ikiwa na alama 37, na ndio msimu ambao walimaliza nafasi ya chini katika misimu mitatu iliyopita ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Kocha wa Mbeya Kwanza, Steven Matata anasema aliyotumwa ameimaliza na hii inakuwa timu yake ya tatu kuipandisha Ligi Kuu baada ya kuipandisha Transit Camp 2004/5 na 2011/12 akiipandisha Tanzania Prisons.