*********************
Na Mwandishi wetu, Babati
MKURUGENZI wa kampuni ya Farm Green Imprements LTD, Dunga Othman amefikishwa Mahakamani na kushtakiwa kwa kujipatia fedha shilingi milioni 58.4 kwa njia ya udanganyifu kuwa atawapa matrekta wakulima watatu wa Wilaya ya Hanang’ ahadi ambayo hakuitekeleza.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu amesema Dunga alikamatwa Tuangoma Dar es salaam na kusafirishwa hadi mjini Babati, kuweza kukabiliana na mashtaka yake katika kesi namba CC.1/2021 inayohusu kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Makungu amesema Dunga amesomewa mashtaka yake na wakili wa TAKUKURU Martin Makani katika mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Manyara Simon Kobelo.
Amesema Dunga amesomewa mashtaka matatu ya kujipatia fedha shilingi milioni 58.4 toka kwa wananchi watatu wa Wilaya ya Hanang’ kwa udanganyifu kuwa atawaletea matrekta ahadi ambayo hakuitekeleza tangu mwaka 2016.
“Uchunguzi wetu umebaini kuwa Dunga alijipatia fedha hizo kupitia kampuni ya Farm Green Imprements LTD kwa ahadi ya kuwaletea matrekta wananchi hao,” amesema Makungu.
Amesema hata hivyo, Dunga hakuwaletea wananchi hao matrekta wala kurejesha fedha, zaidi akaua kampuni ya Farm Green Imprements LTD aliyoitumia kujipatia fedha na kuanzisha kampuni nyingine iitwayo PLANCON (T) LTD.
Amesema baada ya kusomewa mashtaka yake Dunga ameyakana na mahakama ilimpa masharti ya dhamana ambayo ni kuwasilisha Mahakamani fedha taslimu shilingi milioni 29.1 au mali yenye thamani ya shilingi milioni 58.4.
“Aidha ametakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao watamdhamini kwa fungu la dhamana la 29.1 na hadi waendesha mashtaka wetu wanaondoka mahakamani Dunga kufanikiwa kupata dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 27,” amesema Dunga.
Ametoa rai kwa watanzania kuheshimu Katiba na Sheria ambazo wamejiwekea wenyewe na pia wajifunze mafundisho mema katika misahafu inayofundisha kutii mamlaka za Serikali zimewekwa na Mungu (BIBLIA, Warumi 13:1-2.)