Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, akisisitiza jambo wakati akifunga Mkutano wa Kwanza wa mashauriano wa wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa mwaka 2021, uliondaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), jijini Mbeya
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Reuben Nkori, akitoa Taarifa ya Bodi yake kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho (hayupo pichani) katika Mkutano wa Kwanza wa mashauriano wa wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa mwaka 2021, uliondaliwa na Bodi na Bodi hiyo, jijini Mbeya.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Bi. Consolata Ngimbwa, akieleza baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika Bodi hiyo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho (hayupo pichani), kwenye Mkutano wa Kwanza wa mashauriano wa wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa mwaka 2021, uliondaliwa na Bodi hiyo, jijini Mbeya
Makandarasi walioshiriki Mkutano wa Kwanza wa mashauriano wa wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa mwaka 2021, uliondaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho (hayupo pichani) wakati akifunga mkutano huo jijini Mbeya.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Kwanza wa mashauriano wa wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa mwaka 2021, uliondaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), jijini Mbeya
PICHA NA WUU
***********************
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, amevitaka vyama vya makandarasi nchini kuungana ili kuwa na sauti moja itakayowarahisishia kuwasilisha maoni na matakwa yao kwa Serikali.
Hayo ameyasema Waziri huyo jijini Mbeya, wakati akifunga Mkutano wa Kwanza wa mashauriano wa wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa mwaka 2021, uliondaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na kusisitiza kuwa kuungana kwao kutaongeza weledi na uwezo wa rasilimali watu na fedha kwa makandarasi hao na hivyo kuweza kupata kazi mbalimbali.
“Nimeona katika kandarasi kubwa changamoto iliyopo ni kushindwa kupata kazi kwa sababu ya kutokidhi mahitaji ya zabuni, hivyo naomba mjitathmini namna ya kuungana ili kuongeza weledi, hatimaye nanyi mpate hizi zabuni kubwa”, amesema Chamuriho.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Bodi hiyo katika kuhakikisha jitihada za kuwasaidia makandarasi wa ndani zinafanikiwa na kufafanua kuwa katika Bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 ilitenga miradi maalumu mikubwa ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ambayo ilitekelezwa na wakandarasi wazawa.
Mfano wa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Barabara ya Urambo- Kaliua (Km 28) ambapo kwa sasa ujenzi wake umekamilika na Ludewa – Kilosa (Km 24) ambao unaendelea kutekelezwa.
Amewaasa Makandarasi kuchangamkia fursa na kushiriki ipasavyo pindi wanapopata zabuni ya kutekeleza miradi kwa kuifanya kwa ubora, kukamilisha kwa wakati na kwa gharama iliyopangwa.
Kwa upande wake, Msajili wa CRB, Reuben Nkori, ametaja changamoto zinazowakabili Makandarasi nchini kuwa ni pamoja na ukosefu wa mitambo, ukosefu wa mitaji, uwezo mdogo katika kusimamia miradi ya ujenzi na uwezo mdogo katika kusimamia rasilimali watu na rasilimali fedha.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bi. Consolata Ngimbwa amesema kuwa Bodi imeboresha Mfuko wa kusaidia Makandarasi na kuweza kutoa huduma kwa Makandarasi wote wa ndani bila kujali daraja la ushitiri, ambapo kwa sasa unatoa dhamana kuanzia shilingi milioni 100 badala ya shilingi milioni 50 ambazo zilikuwa zikitolewa awali.
Mkutano huo uliobeba Kauli mbiu inayosema kuwa ‘Juhudi za makusudi za wadau, kuwezesha ukuaji wa makandarasi wa ndani’, ni wa kwanza kati ya mikutano minne kwa mwaka huu, ambapo mingine inatarajiwa kufanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza .
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi