Home Mchanganyiko JAFO AWAAGIZA WAKURUGENZI KUSIMAMIA UJENZI WA MADAMPO ILI KULINDA AFYA ZA WANANCHI

JAFO AWAAGIZA WAKURUGENZI KUSIMAMIA UJENZI WA MADAMPO ILI KULINDA AFYA ZA WANANCHI

0

………………………………………………………………………………….

Na.Alex Sonna,Dodoma

WAZIRI wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Selemani Jafo, amewaagiza wakurugenzi wa mikoa ambayo serikali imewekeza kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa madampo ya kisasa kuimarisha usimamizi ili kulinda afya za wananchi.

Jafo,ameyasema leo April 23,2021  jijini Dodoma wakati alipofanya ziara ya kukagua shughuli zinazofanywa katika dampo la kisasa la Chidaya nje kidogo ya jiji la Dodoma.

Jafo amesema kuwa serikali imetumia kaiasi kikibwa cha fedha katika utekelezaji wa miradi hiyo lakini pamekuwa na udhaifu katika usimamizi hali ambayo inatishia afya za wananchi katika maeneo hayo.

Waziri Jafo, amesema kuwa usimamizi katika Dampo la kisasa la Chidaya kwa uogozi wa jiji la Dodoma, unahitajika ili kusaidia kuimarisha afya za wananchi wanaoishi katika maeneo jirani.

“Natoa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi wa jiji la Dodoma kuhakikisha kuwa haya mabwawa ambayo yanahifadhi maji taka yatokanayo na takataka zinazoletwa hapa mjenge ukuta ili kulinda yasivuje kwenda katika mito ya jirani hali inayoweza kuleta madhara kwa wananchi wetu”amesema Jafo

Aidha, amesema kuwa maji hayo yatokanayo na uchafu mblimbali yanaweza kuwa na kiwango fulani cha sumu ambacho kama hakitadhibitiwa vizuri na kuingia katika vyanzo vingine vya maji itakua hatari kwa maisha ya wananchi.

“Naagiza myapime haya maji ili kubaini kiasi gani cha sumu kipo ndani na baadaye myatibu lakini pia suala la kujenga ukuta kulinda haya maji ni la muhimu sana ili yasijeenda katika vyanzo vingine vya maji na watu wakayatumia kwa kunywa”amesema Jafo

Hata hivyo Jafo amesema kuwa  halitakuwa jambo la busara kwa viongozi wa jiji kuacha maji hayo yenye sumu kusambaa kwenda katika maeneo mengine ambayo yanaweza kuleta madhara makubwa.

“Hapa kuna mto mmenambia unapita jirani sasa muhakikishe maji haya yanadhibitiwa ili yasije kuingia kule na wananchi kwenda kuyatumia yakaleta madhara makubwa”amesema

Pia, Waziri Jafo amezindua baraza la kazi la wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Rais na kuwataka watumishi katika ofisi hiyo kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Mhe.Jafo amesema kuwa  watumishi wa umma watakiwa kufanya kazi kwa jitihada ili kuacha alama katika utumishi wao na siyo vinginevyo.

“Tuache kufanya kazi kwa mazoea kila mmoja wetu atimize wajibu wake ili tuweze kuacha alama leo hii katika ofisi zetu kuna watu hata akisafiri hakuna anaye hisi pengo lake hii yote ni kutokana na kuwa hatujafanya kazi za kututambulisha uwepo wetu”amesisitiza

Hata hivyo, Baraza hilo pia limetumika kupitisha bajeti ya Ofisi hiyo itakayo wasilishwa wiki ijayo bungeni jijini Dodoma.