Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi yake kwa Mwaka 2021/22, Bungeni Jijini Dodoma leo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa, akizungumza na Naibu Waziri wa Ofisi yake, Mhe.Deogratius Ndejembi kabla ya kuwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi yake kwa Mwaka 2021/22, Bungeni Jijini Dodoma leo.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwasilisha hoja Bungeni ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi yake kwa Mwaka 2021/22, Jijini Dodoma leo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole akiwasilisha Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka 2021/22, Bungeni Jijini Dodoma leo.
********************************
Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 22 Aprili, 2021
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewahimiza Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha kero na malalamiko ya kiutumishi yaliyo katika majimbo yao ili ofisi yake iweze kuyafanyia kazi.
Mhe. Mchengerwa ametoa wito huo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2021/22 ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ili Bunge liweze kujadili na kuidhinisha.
Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa, amedhamiria kuingoza ofisi yake kupunguza au kuyamaliza kabisa malalamiko ya Watumishi wa Umma na wananchi yanayohusu masuala ya kiutumishi na utawala bora.
Akihimiza ushughulikiaji wa malalamiko ya watumishi, amewaelekeza Waajiri wote, hasa Maafisa Utumishi kuwasilisha madai ya watumishi kwa wakati ili kupunguza mlundikano wa madeni ya watumishi yanayotokana stahili zao.
Ameongeza kuwa, Ofisi yake itaimarisha matumizi ya mfumo wa kushughulikia malalamiko katika Taasisi za Umma ili malalamiko ya watumishi na wananchi yaweze kufanyiwa kazi kwa wakati.
Mhe. Mchengerwa ametoa rai kwa Maafisa Utumishi kushughulikia changamoto za Watumishi wa Umma kwa wakati ili kujenga ari na morali ya watumishi wa umma kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Mwajiri na Afisa Utumishi yeyote atakayeshindwa kutatua kero na malalamiko yaliyo ndani ya uwezo wake, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake”, amesisitiza Mhe. Mchengerwa.
Akiwasilisha taarifa kwa niaba ya kamati yake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole ameishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma ili kuwajengea hali kiutendaji.
Aidha, Mhe. Polepole ameliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya shilingi 727,932,861,000/= kwa ajili utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais-Ikulu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na taasisi zilizo chini yake.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litajadili ili kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2021/22 ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora yaliyowasilishwa Bungeni na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa.