Home Mchanganyiko TBS yawafunda wauzaji wa mafuta ya kula Iringa

TBS yawafunda wauzaji wa mafuta ya kula Iringa

0

Na Mwandishi wetu Iringa

Mkaguzi wa TBS Bw. Ernest Simon amewataka wauzajji wa mafuta ya kula kuacha kutumia chupa za maji zilizokwisha kutumika kufungashia mafuta badala yake kutumia vifungashio sahihi na salama.

Bw, Ernest ametoa wito huo mapema leo wakati wa ukaguzi wa maduka ya bidhaa za chakula na vipodozi katika eneo la Kitanzini , Manispaa ya Iringa.

Bw. Simon amesema wauzaji hawa wa mafuta ya kula wamekuwa wakihifadhi mafuta ya kula katika chupa za maji zilizotumika ambazo usalama wake unatia shaka, pia chupa hizo zinakuwa hazina maelezo ya msingi ya bidhaa husika kama vile ukomo wa matumuzi wa bidhaa, aina ya bidhaa na anuani ya mzalishaji.

Bw. Simon aliwahimiza wauzaji wa mafuta ya kula kusajili majengo wanayohifadhia na kuuza bidhaa hizo ikiwa ni pamoja na kuthibitisha ubora wake na kuyauza yakiwa kivulini.

” TBS imebeba dhamana ya kumlinda mlaji hivyo haitaendelea kuwavumilia wale wote wanaokiuka utaratibu na kuhatarisha usalama wa afya za walaji,” alisisitiza Bw. Simon.

Wakaguzi wa TBS Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wanaendelea na ukaguzi wa bidhaa za chakula na vipodozi mkoani hapa ambapo katika ukaguzi huo wamesajili majengo ya kuuzia bidhaa hizo pamoja na kuuhisha usajili. Pia wamehimizwa kuondoa dukani bidhaa zilizokwisha muda wake wa matumizi, pamoja na kutouza vipodozi vyenye viambata sumu.