Mjumbe wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Dkt. Zena Mabeyo akichangia jambo wakati wa kikao cha Bodi hiyo kilichoikutanisha na Kaimu Katibu Mkuu wa wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACoNGO).
Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Dkt. Richard Sambaiga akizungumza na wajumbe wa Bodi hiyo jijini Dodoma kilichowakutanisha na Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACoNGO) kulia ni Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Vickness Mayao.
Kaimu Katibu Mkuu Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACoNGO) Focus Magwesela akifafanua jambo mbele ya Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kikao chake cha 46 kilichofanyika jijini Dodoma.
Picha Zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
*********************************
Na Mwandishi Wetu Dodoma
Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Dkt. Richard Sambaiga ameliagiza Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACoNGO) uchaguzi wa viongozi kwa mujibu wa sheria ili kuliwezesha kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.
Dkt. Sambaiga ametoa maelekezo hayo Katika Kikao cha 46 cha Bodi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambapo amesema NACoNGO imekuwa ikiomba kuongezewa muda mara kwa mara jambo jambo ambalo limefia mwisho.
Ameitaka NACoNGO kuhakikisha inakamilisha uchaguzi wa viongozi wake kabla au ifikapo tarehe 1 Juni, 2021 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya kisheria.
Akifafanua jambo, Dkt. Sambaiga amesema Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ipo kwa mujibu wa Sheria ina Mamlaka ya kuhakikisha utekelzaji wa Sera ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Kanuni na utandaji kazi wa NACoNGO ikiwa pamoja na kufanyika kwa Uchaguzi wa viongozi wa Baraza hilo.
“Tulishatoa agizo la kwanza mnamo tarehe 31 Machi, 2020 kufanya uchaguzi kuchagua viongozi wenu ndani ya kipindi cha miezi minane lakini hamkutekeleza hilo, … mmekuwa mkiomba kuongezewa muda na hadi sasa unaomba kupewa muda zaidi” alisisitiza Dkt. Sambaiga
Alifafanua kuwa mnamo tarehe 03 Machi, 2021 Bodi iliongeza muda wa siku 14 kutekeleza maagizo hayo lakini bado agizo hili ambalo halikutekelezeka na hivyo kusititiza kukamilika kwa uchaguzi kabla ya tarehe 1Juni, 2021.
Awali akitoa maelezo kuhusu utekelezaji wa maelekezo ya Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Kaimu Katibu Mkuu wa NACoNGO Focus Magwesela alisema Baraza hilo linashindwa kukidhi matakwa ya sheria kutoka na uhaba wa rasrimali fedha.
Baada ya ombi lake la kusogezwa mbele kwa miezi mingine mitano kugonga mwamba, Kaimu Katibu Mkuu huyo wa NACoNGO ameihakikishia Bodi ya NGOs kuwa maelekezo yake yatafanyiwa kazi kama ilivyoelekezwa.
“Niwahakikishie Mheshimiwa Mwenyekiti na wajumbe wa Bodi kuwa tutalifanyia kazi agizo kwa wakati uliotolewa na Bodi yako” Alisisitiza. Magwesela.