Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bw. Donasian Kessy akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam.
******************************
Na Noel Rukanuga, Dar es Salaam.
Taasis ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imeokoa Sh.16,600,000 baada ya kufanya chunguzi mbalimbali katika Saccos pamoja na watu binafsi ambapo fedha hizo zilifanyiwa ubadhirifu kinyume na sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa ripoti ya utekelezaji katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi mwaka huu, Mkuu wa Taasisi ya TAKUKURU Mkoa wa Temeke Bw. Donasian Kessy, amesema kuwa katika kipindi hicho pia wamefanikiwa kufungua kesi tano katika Mahakama tofauti.
Bw. Kessy amesema kuwa miongoni mwa kesi hizo zilizofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo Meneja Mwandamizi Uhasibu wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Philidoni Daudi Siyame Februari 8 mwaka huu alifikishwa mahakamani kwa tuhuma ya kuisababishia Serikali hasara shilingi bilioni 1.4.
“Bw. Siyame ameisababishia serikali hasara kwa kitendo cha kufuta kumbukumbu za upotevu wa vifaa vya umeme kwenye mfumo wa utunzaji wa kumbukumbu za Bohari” amesema Bw. Kessy
Amefafanua kuwa kufanya kosa la kuisababishia serikali hasara ni kinyume na Aya ya Jedwali la kwanza ikisomwa pamoja na kifungu cha 57 (1) na kifungu cha 60(2) cha sheria ya uhujumu uchumi sura ya 200 kama ilivyofanyiwa maboresho.
Bw. Kessy amesema kuwa pia wamefanikiwa kushinda kesi tatu ikiwemo kesi namba CC/608/2019 iliyomuhusu Joseph Lubunza na mwenzake waliyekutwa na hatia chini ya kifungu cha 302 na 100 B cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kwa kujifanya waandishi wa hababri wa kujitegemea.
Bw. Kessy ameeleza kuwa katika kipindi hicho Dawati la Kuzuia Rushwa limefanikiwa kufanya chambuzi za mfumo mitatu kwa lengo la kubainisha mianya ya rushwa katika sekta mbalimbali, ambapo amebainisha kuwa
kumekuwa na hucheleweshaji wa muhtasari wa vikao vya kupitisha vibali vya ujenzi unaosababisha vibali kutoidhinishwa kwa wakati.
“Tumeendelea kuelimisha umma kupitia vyombo vya habari, kuendesha semina 10 kwa makundi mbalimbali na mikutano ya hadhara, mijadala ya wazi lengo ni kuwahamasisha wananchi kushiriki kwa vitendo katika mapambano dhidi ya rushwa kwa ” amesema Bw. Kessy.
Ameeleza kuwa Takukuru Mkoa wa Temeke imeweka mikakati katika kipindi cha mwezi April hadi Juni mwaka huu kuhusu kudhibiti vitendo vya rushwa ikiwemo kuangalia njia bora ya kuweza kutokomeza vitendo vya hivyo katika miradi mbalimbali iliyopo Manispaa ya Temeke.
Bw. Kessy ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kupitia mitandao yote ya simu kwa kupiga au kutuma ujumbe mfupi kwa namba ya bure 113 au kufika ofisi za Takukuru zilizopo karibu.