*************************************
Na Ahmed Sagaff – DODOMA
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Nd. Gerson Msigwa ameomba ushirikiano kutoka kwa uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) katika kutetea maslahi ya waandishi wa habari kwenye vyombo wanavyofanyia kazi ili kuinua hadhi zao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii leo jijini Dodoma mara baada ya kukutana na uongozi huo, Msigwa amesema anafahamu changamoto zinazowakabili waandishi wa habari nchini tangu alipokuwa akifanya kazi hiyo mkoani, hivyo anafahamu kwamba hali ya wanahabari haifurahishi na kwamba anataka kuona wanahabari wananufaika na kazi wanazozifanya.
“Kwa hiyo tumekubaliana kwamba tufanye kazi kubwa ya kuhakikisha tunanyanyuana, tunawekana sawa na tunashirikiana, hatuna muda kwa ajili ya kuvutana, tuna muda kwa ajili ya kushirikiana na kuijenga nchi yetu”, ameeleza Msigwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TEF, Nd. Deodatus Balile amewataka wanahabari kujiendeleza kielimu ili kukidhi vigezo vya kisheria vilivyowekwa miaka mitano iliyopita ambavyo vinainua hadhi ya taaluma ya habari kwa kumtaka mwandishi wa habari kuwa na elimu ya fani hiyo kuanzia stashahada na kuendelea.
“Waandishi ambao watakuwa wamesahau kidogo kwamba Novemba tutakuwa tunafikia muda wa kuanza kutumika ile kanuni ambayo inataka kila mwandishi wa habari kuwa na elimu ya kuanzia stashahada ya uandishi wa habari kwenda juu, kwa hiyo kanuni hiyo inaanza kutekelezwa mwaka huu hivyo ambao hawajaenda kusoma, waende”, amesema Balile.
Kwa mujibu wa kanuni 17 (2) ya Huduma za Habari 2017, anayetaka kusajiliwa kama mwandishi wa habari anapaswa kuwa na stashahada au shahada ya uandishi wa habari kutoka kwenye chuo kinachotambuliwa na Serikali.
Aidha, Serikali ilitoa muda wa miaka mitano ili wanahabari ambao hawana sifa zilizoainishwa kwenye kanuni hiyo, wajiendeleze kitaaluma ili kuendana na matakwa ya kisheria.