Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania Pretoria nchini Afrika Kusini. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Mhe. Meja Generali (Mst) Gaudence Milanzi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Grace Naledi Pandor
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Grace Naledi Pandor
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Mhe. Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini humo
*******************************
Na Mwandishi wetu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Grace Naledi Pandor kujadili mambo ya kuendeleza mashirikiano baina ya Jamhuri ya Afrika Kusini na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Balozi Mulamula amefanya mazungumzo hayo Pretoria nchini Afrika Kusini ambapo pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula alieleza kuwa mahusiano kati ya Afrika Kusini na Tanzania ni ya kihistoria na yameendelea kuimarika tangu enzi a kupigania uhuru kwa nchi za kusini mwa Afrika.
Kwa upande wake Waziri Pandor ameishukuru kwa ujio wa Balozi Mulamula na kwa kufika nchini Afrika Kusini na pia alieleza kuwa Jamhuri ya Afrika Kusini inathamini mashirikiano ya kihistoria kati ya nchi zetu mbili na hivyo kinachohitajika ni kuendeleza na kuimarisha mashirikiano ya kiuchumi na kisiasa tuliyonayo sasa hivi. Jamhuri ya Afrika Kusini inayo azma ya kushiriki kikamilifu kujenga makumbusho ya urithi (heritage museum) ya harakati za kupigania uhuru kusini mwa Afrika zenye chimbuko lake nchini Tanzania na vilevile kuonyesha juhudi za Tanzania katika harakati za kupigania uhuru na kwa nchi za kusini mwa Afrika.
Mawaziri hao wamejadili pia mchakato wa tathimini ya utekelezaji wa Bi-National Commission (BNC) ambapo kwa mwaka huu Afrika Kusini ndiyo itakuwa mwenyeji wa tathimini hiyo ambayo hujumuisha ngazi ya watedaji wakuu wa sekta mbalimbali wan chi hizi mbili, Mawaziri na huitimishwa na Waheshimiwa Marais wa nchi zote mbili.
Aidha, Balozi Mulamula kabla ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, alikutana na watumishi wa ubalozi wa Tanzania Pretoria katika mkutano ulifanyika Ubalozini, Mhe. Waziri alipokea taarifa ya eneo la uwakilishi la Ubalozi ambalo linajumuisha Afrika Kusini, Botswana, Falme ya Lesotho na SADC. Taarifa hiyo ilieleza juhudi za Ubalozi katika kukuza mahusiano na nchi za eneo la uwakilishi, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, diplomasia ya siasa, wanadiaspora wa eneo la uwakilishi.
Balozi Mulamula ameutaka Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini kuendela kufanya kazi kwa malengo, watumishi kujiwekea malengo ili kufanikisha malengo ya Ubalozi na hatimaye Ubalozi kuchangia malengo ya Wizara kwa ujumla.
“Nawasihi kuendeleza mahusiano na nchi za uwakilishi na Balozi nyingine zilizopo katika nchi za uwakilishi na suala hili la kujenga mahusiano na watumishi wote na siyo Balozi pekee yake,” amesema Balozi Mulamula.