***************************
Na Mwandishi wetu, Babati
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Manyara, imempongeza Katibu Tawala wa Mkoa huo Missaile Musa kwa kumchukulia hatua ya kumuondoa kwenye nafasi ya ofisa manunuzi aliyeagiza kuwekwa madirisha yaliyo chini ya kiwango kwenye Ikulu ndogo ya Hanang’.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu ameyasema hayo ofisini kwake mjini Babati wakati akitoa taarifa ya robo tatu ya mwaka kuanzia mwezi Januari hadi Machi mwaka huu.
Makungu amesema hata hivyo ofisa manunuzi huyo Dominicianus Kilina aliyeagiza kuwekwa kwa madirisha hayo yaliyokuwa chini ya kiwango hatashitakiwa kwa sababu Serikali haikulipa fedha zozote.
Amesema Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, RAS Musa amethibitisha kuwa Serikali haikulipa kiasi chochote cha fedha kwa ajili ya madirisha hayo yaliyokuwa chini ya kiwango wakati wa utengenezaji hadi kupachikwa kwake.
“Hivyo hakuna hasara iliyopatikana vinginevyo mhandisi Kilina aliyeagiza kuwekwa kwa madirisha hayo angeshtakiwa kwa kusababishia hasara Serikali kinyume cha sheria ya uhujumu uchumi sura ya 200,” amesema Makungu.
Ameishauri mamlaka nyingine za nidhamu kuiga hatua za Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara kwa kuchukua hatua.
“Kupitia utaratibu huo wa kuwawajibisha ndani ya mamlaka za umma, tutafanikiwa zaidi katika kupambana na rushwa, ubadhirifu wa aina zote kuliko kutuachia TAKUKURU pekee,” amesema Makungu.
Amesema wanamshauri RAS Manyara Missaile Musa amuengue kwenye nafasi ya usimamizi wa miradi mhandisi Kilina kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo katika usimamizi wa miradi na kusababisha kuwekwa kwa vifaa vya ujenzi vyenye ubora hafifu kwenye majengo ya Serikali kama ilivyotokea kwenye mradi wa ujenzi wa Ikulu ndogo ya Hanang’.
“Tumeelekeza pia kwa mamlaka zote za manunuzi Mkoani Manyara, ziwasilishe taarifa ya miradi ya maendeleo waliyopewa dhamana ya kuisimamia mahali ilipo na kiasi cha fedha walizopokea kwa ajili ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi hiyo kuanzia hatua za awali,” amesema Makungu.
Amesema awali, umma wa watanzania ulijulishwa kupitia vyombo vya habari juu ya kushikiliwa kwa mzabuni Gaudensi Joakimu Kauki baada ya kubainika kuweka madirisha yaliyo chini ya kiwango katika ujenzi wa Ikulu ndogo unaoendelea Wilayani Hanang’.
Amesema katika taarifa hiyo umma ulijulishwa mzabuni huyo alipewa zabuni ya kutengeneza madirisha ya Aluminium na ofisi ya manunuzi ya mkoa wa Manyara kwa ajili ya jengo la Ikulu ndogo ya Hanang’.
“Kwa mujibu wa orodha ya kazi, vifaa na gharama (BOQ) mzabuni alitakiwa kutengeneza na kuweka kwenye jengo hilo madirisha ya Aluminium yenye kioo cha unene (thickness) wa 6mm lakini badala yake akatengeneza na kupachika madirisha yenye kioo cha unene (thickness) wa 5mm,” amesema Makungu.
Amesema madirisha hayo yaliyokuwa chini ya kiwango walielekeza yaondolewe kwenye jengo hilo na yaondolewe kwenye jengo hilo na yaondolewa.
Amesema mzabuni huyo tayari ameleta madirisha yenye ubora unaokubalika wa 6mm, wameyakagua na kujiridhisha kuwa yapo sawa hivyo yawekwe kwenye jengo hilo.