Kaimu Afisa Maendeleo Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahanl (kulia) akimkabidhi viazi vitamu Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida, Alhaj Burhan Mlau vilivyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi kwa ajili ya futari ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa Waislamu wa mkoa huo jana.
Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Wilaya ya Singida Vijijini, Amiri Kisuda, akizungumzia msaada huo.
Sehemu ya shehena ya viazi vilivyo tolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Rehema Nchimbi.
Viazi vya futari vikishushwa kwenye gari.
Viazi vya futari vikiingizwa ndani kabla ya kugawiwa waislamu..
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ametoa chakula kwa waumini wakiislamu mkoa huo kama sehemu ya futari katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Akikabidhi msaada huo wa viazi kwa Msikiti wa Kati na Mandewa kwa niaba ya mkuu wa mkoa Kaimu Afisa Maendeleo Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahanl alisema Dkt. Nchimbi ametoa chakula hicho kwa makundi yasiyojiweza ndani ya waumini wa Kiislamu Mkoa huo ili waweze kufuturu na kufanya ibada yao kuwa kamili.
Alisema mkuu wa mkoa anawapongeza Waislamu wote kwa kuwa chachu ya maendeleo na kuuombea mkoa wa Singida na nchi yote kwa ujumla na amewaomba waumini hao kupitia mfungo huo wa Ramadhani kuendelea kumuomba mwenyezi Mungu ili atuepushe na mambo mabaya yakiwemo magonjwa na kumuombea Rais wetu Samia Suluhu Hassan ambaye ana muda mfupi wa kuongoza nchi baada ya aliyekuwa Rais Hayati Dkt. John Magufuli kufariki.
“Wajibu wa viongozi wa dini ni kutuombea sisi na Taifa kama tulivyoona juzi walivyofanya kongamano kubwa la kuombea dini pamoja na Hayati Dkt. Magufuli.” alisema Ndahani.
Aidha wakati akipokea msaada huo wa viazi Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida, Alhaj Burhan Mlau alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwajali Waislamu kwani kila mwaka anakuwa wa kwanza kutoa futari kwa waumini hao.
“Nimpongeze Mama yetu mkuu wa mkoa kila mwaka haachi kutoa futari kwa Waislamu tena mwanzoni kabisa mwa mwezi, mwaka jana alitoa msaada kama huu na hii ni kawaida yake kwa maana miaka yote huwa anatoa futari kwa kumi la kwanza na la pili na kumi la tatu huwa anatoa futari kwa kutuwezesha waislamu hasa walengwa ambao hawana uwezo, wazee, mayatima, masikini, wajane na mafukara nichukue nafasi hii kwa niaba ya waislamu kumshukuru Dkt. Nchimbi kwa sadaka hii Mwenyezi Mungu aendelee kumlinda na familia yake na kumpa moyo huo huo kwani wapo matajiri wengi lakini hawafanyi kama anavyofanya yeye.”alisema Mlau.
Alhaj Mlau alisema atahakikisha futari hiyo inawafikia walengwa ili kwa siku hizo chache waweze kufuturu na kupunguza makali ya mfungo.
Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Wilaya ya Singida Vijijini, Amiri Kisuda alimshukuru Dkt.Nchimbi kwa kuwatia moyo waislamu katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhan na kuwataka watu wengine kuiga mfano huo.
Futari ni mojawapo ya chakula cha kidini ambacho huliwa wakati wa Ramadani na mara nyingi hufanyika na jamii, yaani watu wanakusanyika ili kufuturu pamoja. Futari inachukuliwa tu kabla ya Magharibi, yaani machweo. Waislamu wengi wanaamini kuwa kulisha mtu kamatar kama namna ya sadaka na yenye manufaa sana na kwamba hayo yalifanywa hata na Mtume Muhammad.