Menenja wa SIDO mkoa wa Morogoro, Haika Shayo.
*************************
NA VICTOR MAKINDA. MOROGORO
Shirikala la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Mkoa wa Morogoro, limewawezesha kupata jokofu la asili la kutunzia nyanya na mazao ya mboga mboga sambamba na kuwapatia mafunzo ya usindikaji wa zao la nyanya wakulima wa kata ya Dumila, Wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro.
Akizungumza na wakulima hao Dumila mwishoni mwa wiki, Meneja wa SIDO mkoa wa Morogoro, Haika Shayo, alisema kuwa shirika la SIDO, pamoja na majukumu mengine yenye lengo la kuendeleza viwanda vidogo, lina wajibu wa kutoa huduma ya tenkolojia na ufundi kwa ajili ya kuongeza thamani bidhaa na malighafi mbali mbali zinazozalishwa na wananchi ili ziweze kukidhi vigezo na kuyafikia masoko yenye tija.
“Katika kutekeleza dhana hiyo, tumewawezesha wakulima wa dumila ambao wanajishughulisha na kilimo cha nyanya na mboga mboga kuweza kuwa na jokofu asilia kwa ajili ya kuhifadhi nyanya kwa muda mrefu ili zisiweze kuharibika na kuweza kuyafikia masoko mbali mbali yenye tija.” Alisema Shayo.
Shayo aliongeza kusema kuwa sambamba na hayo, SIDO imewapatia mafunzo wakulima hao ya kusindika nyanya na kutengeneza bidhaa mbali mbali zinazotokana na zao hilo kama vile, Sharobati ya Nyanya, Waini ya Nyanya, Jam, tomato sosi na bidhaa nyingine.
Kwa upande wake, Joan Nangawe, Afisa Uendelezaji wa Tenkolojia ya Chakula (SIDO) mkoa wa Morogoro alisema kuwa Shirika la SIDO, linashiriki programu ya uendelezaji na ukuzaji wa ujuzi hiyo waliandika andiko lililowawezesha kuandaa utengenezaji wa majokofu ya asili katika kupunguza upotevu wa mali mbichi kwa sababu ya kukosa teknolojia za uhifadhi na usindikaji wa mazao hayo
Nangawe alisema kuwa eneo la Dumila ni eneo ambalo linazalisha nyanya na mboga mboga kwa wingi ambapo wakulima walikuwa wakikabiliwa na upotevu mkubwa wa mazao hayo kwa kuwa yalikuwa yakiharibika kabla ya kufikishwa sokoni kwa kukosa eneo maalumu la kuhifadhia ili yadumu kwa muda mrefu.
“ Jokofu hili lina uwezo kuhifadhi nyanya tani moja sambamba na mboga mboga nyinginezo na zinaweza kukaa humu kwa muda wa siku 14 pasipo kuharibika, hivyo unaweza kuona ni kiasi gani wakulima hawa wanaweza kuokoa uharibifu wa mazao yao wakati wanasubiri kusindika au kupeleka sokoni” Alisema Joan”.
Joan alisema Jokofu hilo linatumia teknolojia ya kiasili kwa kutumia malighafi za gharama nafuu, ana uhakika kuwa wakulima wa Dumila na maeneo mengine mkoani Morogoro watapata mwamko wa kujifunza na kuitumia teknolojia hiyo ili waweze kuhifadhi mazao yao ya mboga mboga kwa muda mrefu.
Akitoa Shukrani zake kwa Shirika la SIDO kwa niaba ya kikundi cha wazalishaji wa zao la nyanya na mboga mboga cha Dumila, Mwenyekiti wa kikundi hicho, Mpondomoka Ramadhani alisema kuwa SIDO imewasidia kurudisha matumaini yao ya kuzalisha kwa tija na kupata masoko ya uhakika hivyo watakuza vipato vyao na kuboresha hali zao za maisha.
“ Kipindi cha msimu wa mavuno ya nyanya hapa kwetu Dumila,tulikuwa tunapata hasara kubwa kwa kuwa nyanya nyingi huozea shambani kwani huwezi kuvuna kama huna soko na ikiwa utavuna hakuna pa kuzihifadhi ili zisiharibike pia hatukuwa na ujuzi wa usindikaji”.
Ramadhani aliongeza kusema kuwa wanalishukuru shirika la SIDO kwa kuwapatia elimu ya kusindika zao la nyanya na kuwasaidia kupata jokofu ambalo kwao ni mkombozi mkubwa kwa kuwa wana uhakika sasa mazao yao hayataharibika