Waziri wa Nishati Mhe. Dkt Medard Kalemani kulia akipokea ripoti ya kamati ya makubaliano ya ujenzi wa bomba la mafuta kati ya nchi mbili za Tanzania na Uganda kutoka kwa Katibu wa Kamati hiyo Leornad Masanja, kukamilika kwa makubaliano hayo sasa ujenzi wa bomba hilo unaanza.
Waziri wa Nishati Mhe. Dkt Medard Kalemani akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya ripoti ya makubaliano ya ujenzi wa bomba la mafuta kutoka nchini Uganda hadi Tanga Tanzania, kutoka kwa kamati maalumu iliyoundwa, kukamilika kwa makubaliano hayo sasa ujenzi wa bomba hilo unaanza.
Katibu wa kamati ya makubaliano ya ujenzi wa bomba la mafuta kati ya nchi mbili Uganda na Tanzania, Leonard Masanja akizungumza mara baada ya kukabidhi taarifa ya ripoti hiyo, kukamilika kwa makubaliano hayo sasa ujenzi wa bomba hilo unaanza.
…………………………………………………………………..
Na Ezekiel Mtonyole- Dodoma.
Serikali Tanzania imepokea taarifa ya ripoti ya kamati ya majadiliano kati ya nchi ya Uganda na Tanzania kwa ajili ya makubaliano ya ujenzi wa mradi wa bomba kubwa la mafuta linaloanzia Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Mkoani Tanga hapa nchini.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya ripoti hiyo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Waziri wa Nishati Dkt.Medard Kalemani amesema kukamilika kwa majadiliano hayo sasa mradi utaanza kutekelezwa haraka sambamba na kuanza kwa zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaopitiwa na mradi fidia inayofikia bilioni 28.8.
“Tumepokea kwa niaba ya Serikali taarifa ya makubaliano ambayo yamefanyika kwa zaidi ya miaka miwili unaweza kuona kazi ilivyokuwa ngumu, tunaelewa kazi iliyofanyika ni kubwa ya mradi huu wa ushirika wanchi mbili ambayo mkataba wake ulisainiwa May 26, 2017 kati ya Rais wa Uganda na hayati Dkt John Magufuli” amesema Dkt Kalemani.
Amesema mara baada ya kukamilika kwa majadiliano hayo sasa kazi ya ujenzi wa bomba hilo utaanza haraka huku akibainisha kuwa kuna baadhi ya kazi zilianza tangu kusainiwa kwa mkataba huo kazi hizo ni kutambua ardhi ambako bomba hilo litapita na kupata kilomita 1445 kwa pande zote mbili Uganda na Tanzania.
Pia amesema mradi huo ni wa kwanza kwa urefu ambapo bomba linaupana wa inchi 24, wa mafuta ya kuchemsha na kwamba bomba litapita katika Mkoa 8, Wilaya 24, vijiji 124, na vitongoji zaidi ya 300 huku ukitarajiwa kunufaisha watanzania wengi kupitia fursa za ajira ambapo kwa kazi za awali wataajiriwa wafanyakazi zaidi ya elfu kumi(10,000).
“Jambo la muhimu sana ni la watanzania kuchukua fursa za kiuchumi,watakaoajiriwa ni zaidi ya elfu kumi na kwa mujibu wa Sheria za uwekezaji watanzania zaidi ya asilimia 80 ndio watakaoajiriwa kwenye ujenzi huo huku kazi zote zitafanywa na watanzania ila hawatachukuliwa kiholela bali watashindanishwa,” amesema.
Kutokana na hayo Waziri Kalemani ametoa rai kwa wananchi wanaopitiwa na mradi huo kupisha eneo mara baada ya malipo ya fidia ili kurahisha shughuli za ujenzi kuendelea.
“Serikali zote mbili yaani Tanzania na Uganda zimetoa kiasi cha pesa kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi wanaopitiwa na mradi huo,hivyo wale wanaohusika na ulipaji wa fidia hizo wanapaswa kuwa makini ili kuondokana na malalamiko kutoka kwa wananchi,” amesema.
Licha ya hayo ameeleza shughuli zitakazofanyika katika mradi huo ni pamoja na kujenga makambi 16 ,maeneo ya kulainisha chuma,kujenga maeneo ya kuweka matanki ya mafuta pia mradi huo utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kupitisha mapipa 216,000 ya mafuta kwa siku na kwamba pipa moja la mafuta litalipiwa kiasi cha Dolla za Kimarekani 12.77 kwa siku.
“Tunafungua ukurasa mpya,sasa tuache maneno na Sasa kazi inayofuata ni kwenda kufanya kazi,majadiliano yamekamilika kwa mafanikio makubwa,na kwa vile majadiliano yamekamilika kazi inatakiwa kuanza haraka iwezekanavyo,” amesema.
Katika hatua nyingine Waziri Kalemani amemteua msimamizi wa mradi huo ambaye anatoka shirika la maendeleo ya petroli nchini (TPDC) Asiadi Mrutu na Mratibu msaidi wa mradi huo Chisamalwa Nyang’ao ambapo atasimamia uundwaji wa timu maalumu ya usimamizi wa mradi huo na kuwataka kufanya kazi kwa bidi na mara baada ya kuanza ujenzi, ujenzi usizidi miaka mitatu.
Licha ya hayo ameeleza shughuli zitakazofanyika katika mradi huo ni pamoja na kujenga makambi 16, maeneo ya kulainisha chuma na kujenga maeneo ya kuweka matanki ya mafuta.
Awali Katibu wa kamati ya majadiliano ambaye pia ni Katibu mkuu Wizara ya Nishati Leonard Masanja amesema timu ya majadiliano imefanya uchunguzi na kwamba Ujenzi unatarajiwa kuanza Wakati wowote kuanzia Sasa.
“Ujenzi wa mradi utachukua miaka mitatu,hatutegemei zaidi ya hapo na lazima tuipongeze Serikali yetu kwa kushirikiana na Uganda kwa kukubali Kutoa fedha kufidia maeneo ambayo Wananchi wamepitiwa na ujenzi,” amesema Masanja.