Home Mchanganyiko MBUNGE SANGU AITAKA SERIKALI KUANZA UJENZI WA BARABARA YA KILYAMATUNDU HADI MAJIMOTO...

MBUNGE SANGU AITAKA SERIKALI KUANZA UJENZI WA BARABARA YA KILYAMATUNDU HADI MAJIMOTO KWA KIWANGO CHA LAMI

0

MBUNGE wa Kwela (CCM), Deus Sangu,akiuliza swali bungeni Dodoma kuhusu ujenzi wa barabara kwa kiwango cha Lami ya kilometa 200 ya Kilyamatundu hadi Majimoto inayounganisha Mkoa wa Rukwa na Songwe.

………………………………………………………………………….

Na.Alex Sonna,Dodoma

MBUNGE wa Kwela (CCM), Deus Sangu ameitaka serikali kuanza ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya kilometa 200 katika kutoka Kilyamatundu hadi Majimoto ambayo inaunganisha Mkoa wa Rukwa na Songwe.

Akiuliza maswali bungeni leo, April 19,2021 bungeni Dodoma,Mbunge huyo ametoa angalizo kwa Wizara ya Ujenzi kuwa mtaalamu aliyepo eneo la mradi kasi yake ni ndogo sana na kutaka amalize kazi hiyo ndani ya kipindi cha mkataba.

“Kwa kuwa barabara kutoka Mji mdogo wa Laela kupitia Mlokola hadi kuunganisha nchi jirani ya Zambia ni ahadi aliyotoa Rais wakati wa kampeni, na wananchi wapo tayari kuachia eneo la barabara kutokana na umuhimu wa barabara hiyo, naomba kujua lini barabara hii itafanyiwa upembuzi yakinifu ili ijengwe kwa kiwango cha lami,”amehoji.

Pia, amesema Hayati Dk.John Magufuli akiwa kwenye ziara Mkoa wa Rukwa aliahidi ujenzi wa barabara kutoka Kaengesa hadi Chitete na tayari upembuzi yakinifu umekamilika, na kuhoji lini ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami utaanza.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya amesema kuwa barabara ya Kilyamatundu – Muze – Mfinga – Kasansa hadi Majimoto yenye urefu wa kilometa 206 ni barabara ya mkoa inayosimamiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).

Amesema kuwa barabara hii inaunganisha mkoa wa Rukwa na mkoa wa Songwe eneo la Kilyamatundu na Kamsamba katika daraja la Momba.

“Kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hiyo, Serikali ilianza kuchukua hatua za kuimarisha barabara hii kwa kuanza na kukamilisha ujenzi wa daraja la Momba lenye urefu wa mita 84 na barabara za maingilio zenye urefu wa kilometa 1.2 ambalo lilikuwa ni kikwazo kikubwa cha mawasiliano baina ya mikoa ya Rukwa, Katavi na Songwe,”amesema.

Aidha ,amesema serikali inaendelea na kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Ntendo – Muze – Kilyamatundu ambao unahusisha sehemu ya Kilyamatundu – Muze yenye urefu wa kilometa 142. Kazi ya usanifu imefikia asilimia 50.

Amebainisha kuwa mara usanifu wa kina utakapokamilika, maandalizi ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami yataanza kulingana na upatikanaji wa fedha.

Pamoja na hayo, amemhakikishia Mbunge huyo wamechukua ushauri wake na kumuagiza Meneja wa Tanroads kusimamia mtaalam huyo ili kukamilisha ndani ya mkataba.

“Pia Kaengesa kwenda Kitete barabara hii yenye urefu wa kilometa saba ni ahadi za viongozi wa kitaifa nimuahidi ahadi zote zilizoahadiwa zitatekelezwa kama zilivyoahidiwa na ukianza upembuzi yakinifu ni hatua ya utekelezaji wa ahadi hiyo na zitajengwa kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha,”amesema.